Sababu za Ndugai kutaka kuwajibu CAG, Halima Mdee hizi hapa

Muktasari:

  • Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai leo Jumatatu Januari 7, 2019 atakutaka na waandishi wa habari mjini Dodoma kujibu kauli iliyotolewa na CAG, Profesa Mussa Assad kuwa Bunge ni dhaifu na kuungwa mkono na mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai leo Jumatatu Januari 7, 2019 atakutaka na waandishi wa habari mjini Dodoma kujibu kauli zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Kwa mujibu wa taarifa za Bunge iliyotolewa leo Jumatatu, wawili hao wanadaiwa kusema kuwa chombo hicho cha Dola ni dhaifu.

Miongoni mwa kauli hizo ni ile iliyotolewa hivi karibuni na Profesa Assad alipokuwa akihojiwa na idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Alichosema CAG

Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

CAG alijibu: "Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

"Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa."

Akiendelea kufafanua jibu lake, CAG Assad alisema: "Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua."

 

Mwaka 2018  lilipoibuka suala upotevu wa Sh1.5 trilioni kwenye hesabu za Serikali mwaka wa fedha 2016-2017, Assad aliulizwa kuhusu nini kifanyike, akataka Bunge liulizwe kwani ndilo lenye kutakiwa kuibana Serikali kuhusu kutoonekana kwa fedha hizo.

Alichokisema Mdee

Baada ya kauli hiyo ya Profesa Assad, wiki iliyopita Halima Mdee alihojiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu alichokisema CAG na kukubaliana na hoja zake.

Akizungumza leo na Mwananchi Mdee amesema, “Nasubiri kumsikia Ndugai anasemaje. Najua atakuwa anazungumzia kile ambacho alikisema Assad, na mie kukubaliana naye.”