Vijana 30 waepushiwa adha mikataba ya bajaji
Baadhi ya bajaji ambazo zimetolewa kwa vijana ambao ni madereva bajaji katika manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Hatua hiyo inaelezwa kuwa itasaidia kuongeza ajira, kuimarisha huduma za usafiri na kuchochea maendeleo ya uchumi wa wananchi kupitia umiliki wa bajaji kwa masharti yanayowezesha vijana kujitegemea.
Moshi. Zaidi ya vijana 30 katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamepatiwa mikopo ya bajaji kupitia ushirikiano wa Akibabot Saccos na Benki ya Equity, hatua inayolenga kuwaondoa kwenye mikataba kandamizi ya wamiliki wa vyombo hivyo na kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Akizungumza leo Jumapili Julai 12, 2026 wakati wa kukabidhi bajaji hizo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Bodaboda na Bajaji Manispaa ya Moshi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Akibabot Saccos Mkoa wa Kilimanjaro, Hamad Bendera, amesema mpango huo umeanzishwa baada ya kubaini vijana wengi walikuwa wakifanya kazi chini ya mikataba yenye masharti magumu ambayo iliwanyima fursa ya kumiliki vyombo vyao vya kazi.
Amesema kupitia makubaliano kati ya Saccos hiyo na Benki ya Equity, vijana sasa wanapata mikopo kwa masharti nafuu na mchakato rahisi.
"Lengo letu ni kuwapa vijana nafasi ya kumiliki bajaji zao na kuwaondoa kwenye mikataba kandamizi. Tunawahamasisha vijana wengi zaidi kujiunga na Saccos ili wanufaike na mpango huu," amesema Bendera.
Amesema hadi sasa zaidi ya bajaji 30 zimetolewa na matarajio ni kuongeza idadi hiyo kadri mahitaji yanavyoongezeka.
Mmoja wa wanufaika, Detus Shimamwi amesema mpango huo umewapa matumaini ya kujikwamua kiuchumi baada ya muda mrefu wa kufanya kazi chini ya mikataba isiyokuwa na manufaa.
"Awali tulikuwa tunalipa fedha nyingi kila siku kwa wamiliki wa bajaji bila uhakika wa kumiliki chombo hicho. Kupitia mkopo huu marejesho ni nafuu na yanatupa fursa ya kufanya kazi kwa utulivu huku tukijenga umiliki wa bajaji yetu," amesema.
Mnufaika mwingine, Hassan Ally amesema mpango huo utawasaidia vijana wengi kuongeza kipato na kupunguza utegemezi wa mikataba ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiwazuia kujiendeleza kiuchumi.
Meneja Biashara wa Benki ya Equity, Tawi la Moshi, Marik Mollel amesema benki hiyo imeendelea kuweka mkazo katika kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia mikopo yenye masharti nafuu.
Amesema hadi sasa zaidi ya vijana 30 wamenufaika na mpango huo, ambao pamoja na kuinua kipato cha wanufaika unachochea ukuaji wa ujasiriamali na uchumi wa jamii.
Kaimu Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mkoa wa Kilimanjaro, Subira Valerian amesema ushirikiano kati ya Latra, Akibabot Saccos na Benki ya Equity umefungua fursa mpya kwa vijana kumiliki vyombo vyao vya kazi.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira, kuimarisha huduma za usafiri na kuchochea maendeleo ya uchumi wa wananchi kupitia umiliki wa bajaji kwa masharti yanayowezesha vijana kujitegemea.