Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bodaboda, bajaji juu kwenye usajili, kusababisha ajali

Muktasari:

  • Takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) zinaonyesha kuwa mwaka 2025 kulikuwa na ongezeko la utoaji wa leseni za usafirishaji kwa zaidi ya asilimia 89.4 ukilinganisha na zilizokuwapo mwaka uliotangulia.



Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, pikipiki na bajaji zimekuwa sehemu muhimu ya mfumo wa usafiri nchini Tanzania.

Kuanzia mijini hadi vijijini, vyombo hivi vimebadilisha namna wananchi wanavyofika maeneo mbalimbali kwa haraka huku vikitoa ajira kwa maelfu ya vijana na kurahisisha shughuli za biashara.

Kutokana na mahitaji hayo, uwekezaji katika eneo hilo  nao umezidi kuongezeka, kama Takwimu za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) zinavyoonyesha, kuwa mwaka 2025 kulikuwa na ongezeko la utoaji wa leseni za usafirishaji kwa zaidi ya asilimia 89.4 ukilinganisha na zilizokuwapo mwaka uliotangulia.

Leseni zilizotolewa kwa vyombo hivyo ziliongezeka kutoka 63,089 mwaka 2024 hadi 119,461 mwaka 2025. Hili ni ongezeko kubwa kuliko lililoonekana kwenye aina nyingine za vyombo vya usafiri wa kibiashara.

Hata hivyo, pamoja na mchango wake mkubwa katika kurahisisha usafirishaji, pikipiki hizo na bajaji zimeendelea kuwa chanzo kikuu cha ajali nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za Latra, mwaka 2025 kulikuwa na ajali 322 zilizohusisha pikipiki na bajaji ikilinganishwa na ajali 383 mwaka 2024. Ingawa hii ni pungufu ya asilimia 15.9, idadi hiyo bado ni kubwa ikilinganishwa na vyombo vingine vya usafiri.

Ajali hizo zikilinganishwa na vyombo vingine vya moto, inabaki kuwa juu kwani mabasi ya abiria yaliyosababisha ajali 270 na magari ya mizigo yaliyosababisha ajali 237 mwaka 2025.

Kwa upande wa ajali za mabasi ya abiria, takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2024 zilikuwa 303 ambazo zilishuka hadi kufikia 270 mwaka jana huku ajali za magari ya mizigo zikitoka 254 hadi 237 mwaka jana.

Kwa mujibu wa ripoti ya Latra iliyonukuliwa katika kitabu cha hali ya uchumi, ongezeko la usafiri kwa vyombo hivyo vya moto umesababishwa na kukua kwa shughuli za biashara, kuongezeka kwa wawekezaji wapya pamoja na juhudi zinazoendelea kutekelezwa.

“Pia ongezeko hili limesababishwa na juhudi za Latra ikiwemo kutoa elimu kwa umma, kuongeza idadi ya watumishi, kuimarisha na kufanya kaguzi mara kwa mara, na kufungua ofisi katika mikoa yote nchini na katika wilaya za kimkakati ili kusogeza huduma karibu na wananchi,” imeeleza.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo inafafanua kuwa kupungua kwa idadi ya ajali za vyombo vya moto kati ya mwaka 2024 na 2025, ulitokana na kuendelea na kaguzi za mara kwa mara barabarani.

“Hilo limeenda sambamba na madereva kuzingatia sheria, matumizi ya mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi ya masafa marefu pamoja na elimu iliyotolewa kwa wadau wa vyombo vya usafiri barabarani,” imeelezwa.

Akizungumzia suala hili, Mathayo Mathayo ambaye ni dereva wa daladala amesema ongezeko la pikipiki na bajaji linatokana na kuonekana ni usafiri wa haraka kuliko magari.

“Sasa changamoto inakuja na ongezeko la vyombo hivi ni kukosekana kwa umakini, bodaboda na bajaji muda wote wamekuwa na tabia hatarishi barabarani, ambazo zinafanya sisi madereva wa magari kuongeza umakini zaidi, vinginevyo tutasababisha ajali kila siku,” amesema.

Alizitaka mamlaka husika kukahikikisha ukuaji huo unaendana na usalama wa watumiaji wa vyombo hivyo na barabara kwa ujumla.

“Bila hatua madhubuti za kuimarisha nidhamu ya madereva, mafunzo na utekelezaji wa sheria, vyombo hivi vitaendelea kuwa suluhisho la usafiri linalokuja na gharama kubwa za maisha ya wananchi,” amesema.

Hayo yamebainika siku chache tangu taarifa ya Moi ieleze kuwa ajali za barabarani zimeendelea kuongezeka na kuwa kati ya asilimia 60 hadi 62 ya wagonjwa wanatokana na ajali za barabarani.

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti Moi, Dk Joel Bwemelo aliyasema hayo Aprili 22, 2026 jijini Arusha katika mafunzo maalumu ya usalama wa miundombinu ya barabara nchini kwa wahandisi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), wahandisi kutoka sekta binafsi na wadau wengine.

Amesema kati ya ajali hizo, pikipiki (bodaboda) zimechangia asilimia 41 ya majeruhi hao.

"Wagonjwa hao wakifika kwetu mara nyingi huwa na majeraha makubwa ya kichwa, shingo, mgongo na mifupa mirefu, ni wagonjwa wanaopata majeraha makubwa, hali inayosababisha vifo au ulemavu wa kudumu," amesema.

Kutokana na hali hiyo, amesema wataalamu wa afya wameamua kutoka nje ya vyumba vya upasuaji na kushirikiana na jamii kutoa elimu ya usalama barabarani ili kupunguza ajali.

Akizungumzia suala hilo kwa mtazamo wa uchumi, Profesa Haji Semboja amesema kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri huo ndiyo sababu inayofanya usajili wake kuongezeka.

Hata hivyo, vyombo hivi mara nyingi vipo katika nchi zinazoendelea tofauti na nchi ambazo zimekuwa zikitumia magari sana.

Amesema ukiwa na uchumi mzuri na maendeleo ya taknolojia vyombo hivyo havitahitajika kwa sababu watu watapanda magari makubwa, mfano nchi kama Marekani.

“Hii inahusiana na watu maskini na huwezi kuja na sera ambayo inakinzana na mahitaji ya watu wengi. Hii ni fursa ya ajira kwa vijana, zimepunguza muda wa kukaa barabarani, imesaidia usafirishaji. Huenda Serikali haijui kuwa zipo ngapi,” amesema.

Amesema tatizo ni madereva hao kutopitia shuleni kujua namna ya kuviendesha, namna ya kubeba abiria au namna ya kuzingatia sharia, hata wakiwa katika makutano ya barabarani. 

“Lakini wanapata kipato, kuna watu wamejikusanya wanafanya mambo mazuri yanayoongeza uchumi wao wa kila siku na wengine kupata sifa za kukopesheka. Hivyo ni vyema kuwapo kwa sheria na taratibu ili kuhakikisha biashara hii inafanyika kwa kufuata taratibu ikiwemo kupata elimu,” amesema.


Nini kifanyike

Balozi wa usalama barabarani, Ramadhani Msangi amesema miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la njia nyingi za usafirishaji na kuzalisha ajira kwa vijana, lakini changamoto iliyopo ni kutokuwapo kwa mazingira yaliyokuwa yameandaliwa ili kuifanya sekta hiyo kuleta manufaa badala ya matatizo.

“Tunachoweza kufanya ni kuhakikisha sheria inaandaliwa kufanya sekta hiyo kuwa rasmi, kuhakikisha watu wanaotoa mikataba kwa vijana wajulikane, ili wanaoajiriwa wajulikane wana sifa zipi na kama wanafaa kuingia barabarani, mikataba iwe na vipengele gani, ili kuhakikisha haimbani tu dereva bali hata mmiliki,” amesema Msangi ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa elimu, habari na mahusiano wa Road Safety Ambassadors (RSA).

Amesema hatua hiyo itapunguza hatari barabarani na watu watajifunza huku kukiwepo sheria mahususi za bodaboda badala ya kutumia sheria ya usalama barabarani kwa ujumla.

“Pia usimamizi ni muhimu kwa kuwajua wako madereva hao wangapi na wanapatikana wapi, tukishirikiana na serikali za mitaa ambako ndiko vijiwe hivi vya bodaboda vinapatikana, itasaidia,” amesema.