Prime
Kicheko na maumivu ya bodaboda, bajaji za mkataba

Katika miaka ya hivi karibuni, mfumo wa vijana kumiliki pikipiki kupitia mikataba ya malipo ya awamu kati yao na wamiliki wa vyombo hivyo umeenea kwa kasi. Mtindo huu, unaojulikana maarufu mitaani kama "bodaboda za mkataba", umeonekana kuwa njia rahisi inayowasaidia vijana kumiliki vyombo vya usafiri kama pikipiki au bajaji, na hivyo kujitegemea kiuchumi.
Hata hivyo, licha ya kuwa na manufaa mengi, mtindo huu umebeba sura mbili tamu na chungu ambazo, iwapo changamoto hazitashughulikiwa, kwa kiasi fulani zinaweza kuathiri mustakabali wa kundi la vijana wanaoingia katika mikataba hiyo.
Bodaboda ya mkataba hufanyika kwa utaratibu ufuatao: Kijana asiye na uwezo wa kifedha kununua chombo cha usafiri, kwa mfano pikipiki, huingia makubaliano na mtu mwingine mwenye uwezo wa kumiliki chombo hicho. Kupitia makubaliano hayo, kijana hupewa pikipiki aendeshe kwa kipindi maalum, huku akiendelea kulipa fedha kwa awamu hadi deni la chombo litakapomalizika.
Mikataba hii huweka masharti ya malipo ya kila siku, wiki au mwezi, kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili kutegemeana na makubaliano. Baada ya kipindi hicho, na baada ya kulipa deni lote, kijana anakuwa mmiliki rasmi wa pikipiki au bajaji husika.
Mfumo huu hujenga nidhamu ya kifedha kwa vijana, kwani hulazimika kupanga matumizi yao kwa uangalifu ili kutimiza malipo ya mkataba huku wakijikimu kimaisha. Ni hatua ya mwanzo ya kuwafundisha vijana kuhusu biashara, uwajibikaji wa kifedha na kupanga kwa ajili ya maisha ya baadaye.
Pamoja na fursa hiyo, changamoto zimeibuka. Kwa kuzingatia mazingira halisi, mikataba mingi hufanyika kwa mdomo au maandishi yasiyo rasmi na yasiyo na nguvu ya kisheria. Hali hii huwafanya vijana kuwa hatarini pale ambapo kuna migogoro, kwani hakuna ushahidi wa kisheria wa kuwatetea.
Vilevile, masharti ya malipo mara nyingi hayaangalii hali halisi ya kipato cha dereva. Mathalani, kijana hupewa masharti ya kulipa Sh10,000 kwa siku kwa muda wa miezi 15, bila kujali kama amepata wateja au amepatwa na matatizo ya kiafya. Akichelewa au kushindwa kulipa, chombo kinachukuliwa tena bila kurejeshewa hata sehemu ya fedha alizokwisha kulipa. Wengine huishia kupoteza kila walichojitahidi kuwekeza.
Zaidi ya hayo, mfumo huu hauna kinga dhidi ya madhara kama ajali au magonjwa. Ikitokea kijana ameumia au kuugua, hana bima wala msaada wa dharura, lakini bado anapaswa kuendelea kulipa deni la mkataba. Kwa baadhi yao, hali hiyo imekuwa janga kubwa wamerudi mitaani wakiwa mikono mitupu, wakiwa wamejeruhiwa na kubeba madeni yasiyolipika.
Ili mfumo huu uwe na tija na ulinzi wa haki za wahusika wote, kuna haja ya kuweka utaratibu rasmi wa mikataba ya bodaboda kwa kushirikisha taasisi za kifedha, serikali za mitaa, na mashirika ya vijana.
Mikataba iandikwe kwa mujibu wa sheria au utaratibu unaokubalika, ikieleza wazi muda wa mkataba, kiwango cha malipo, masharti ya kiusalama, na jinsi ya kushughulikia changamoto kama ajali, ugonjwa au kushindwa kulipa kwa muda mfupi.
Vijana pia wanapaswa kupewa elimu ya kifedha, maarifa ya usimamizi wa biashara ndogo ndogo, na ufahamu wa haki zao za kisheria kabla ya kuingia kwenye mikataba ya namna hii. Serikali kwa kushirikiana na taasisi za fedha zinaweza kuanzisha mikopo yenye masharti rafiki kwa vijana itakayowezesha kumiliki vyombo vya usafiri kuwawezesha kuepuka na baadhi ya mazingira kandamizi.
Bodaboda za mkataba ni fursa iliyojaa matumaini, lakini iwapo itasimamiwa kwa weledi na busara. Jamii, serikali, na taasisi binafsi zina jukumu la kuhakikisha kuwa mfumo huu unajenga tija nzuri, na matumaini ya kujikwamua kiuchumi.
Kwa sababu mwisho wa siku, kila kijana anayepanda pikipiki hiyo si tu anasaka hela, bali pia anasaka heshima na mustakabali bora wa maisha yake.