Samia Suluhu mgeni rasmi tuzo za fasihi Afrika

Muktasari:

  • Makamu wa Rais,  Samia Suluhu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tuzo za mashindano ya fasihi Afrika zinazotarajiwa kutolewa Februari 15, 2019 ambako washindi wawili kila mmoja hupata Sh11.6 milioni.

Makamu wa Rais Samia Suluhu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tuzo za mashindano ya fasihi ya Afrika zinazotarajiwa kutolewa Ijumaa Februari 15, 2019  katika ukumbi wa Mlimani City jijini hapa.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Februari 11, 2019 na  Isamba Kasaka ambaye ni mkuu wa masoko wa kampuni ya utengenezaji vifaa vya ujenzi ya Alaf Tanzania ambao ni miongoni mwa wadhamini wa shindano hilo.

Kasaka amesema mashindano hayo ya uandishi wa ushairi na riwaya kwa lugha ya Kiswahili huhusisha wanafunzi wote wa vyuo vikuu vilivyopo Afrika na awamu hii kazi 116 ziliwasilishwa.

"Sisi tunadhamini tuzo hizi za fasihi ya kiswahili kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za kukuza na kuendeleza lugha ya kiswahili katika bara la Afrika na dunia kwa ujumla,"amesema Kasaka.

Amewataja washindi watakaopewa tuzo siku hiyo kuwa ni Ngumbau Julius raia wa Kenya ambaye ni mshindi kwa upande wa ushairi kwa shairi lake linaloitwa Moto wa kifuu na Mtanzania Zainab Baharoon kwa upande wa riwaya kwa riwaya yake iitwao Mungu hakopeshwi.

Aidha kila mshindi wa tuzo hiyo atapeawa zawadi ya Dola za Kimarekani 5,000 sawa na Sh11.6 milioni.