Samia atoa sababu za kung’olewa bosi wa Nemc

Muktasari:

  • Kutokana na kuwapo kwa malalamiko ya Nemc ikiwamo ucheleweshaji vibali, kukithiri kwa ubadhirifu Serikali imeanza utekekezaji wa kuisuka upya ikiwamo uteuzi wa bodi na mkurugenzi mpya uliokwishafanyika.

Dar es Salaam. Serikali imesema katika kuhakikisha inakabiliana na urasimu wa Baraza la Mazingira (Nemc) ambao umekuwa ukilalamikiwa kila kona ndiyo maana imeteua mkurugenzi mpya, Samuel Mafwenga.

Akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya madini leo Jumatano Januari 23, 2019 kwenye mkutano mkuu wa kisekta, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema miongoni mwa kazi za mkurugenzi huyo mpya ni kuisuka upya Nemc ili iachane na ubadhirifu huo.

Amesema wachimbaji wadogo wanakabiliwa na vikwazo kama vile ucheleweshaji wa kutolewa cheti cha mazingira kwa wawekezaji, gharama kubwa ya kufanya tathmini ya athari za mazingira kwa wachimbaji wadogo na wa kati, kutokutambuliwa kwa cheti cha utunzaji mazingira kwa wachimbaji wadogo na Nemc na kutopata huduma ya moja kwa moja kutoka kwao.

"Kwa upande wetu tumeshachukua hatua kadhaa ikiwamo kuisuka upya taasisi kwa kumchagua mkurugenzi mpya wa Nemc na mwenyekiti wa bodi na wajumbe wake ili waweze kuzipitia hizi changamoto kwa haraka na kutoa majawabu," amesema Suluhu na kuongeza.

"Tayari nimeanzisha kanda sita ikiwamo ya Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya, Mwanza, Dodoma na Arusha ili kuwafikia wadau wengi zaidi,” amesema.

Amesema kwa kipindi hiki ambacho bado hawajapata elimu Nemc itakuwa mlezi kwa kutoa elimu kabla ya kutoa adhabu.

"Kutojua sheria si kinga ya adhabu, lakini kwa sasa tunawaelimisha kwanza, kumhukumu mtu kabla ya kumpa elimu ni kumuonea," amesema Suluhu.