Serikali kutumia mashahidi 54 kesi ya Kitilya

Tuesday February 12 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwanachi. [email protected]

Dar es Salaam. Serikali inatarajia kuita mashahidi 54 pamoja na vielelezo 218 katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne.

Katika mashahidi hao 54 wanaotarajia kutoa ushahidi katika Mahakaka Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, yupo Waziri wa zamani wa Fedha, Mustafa Mkulo na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema.

Idadi hiyo ya mashahidi na vielelezo imebainishwa na upande wa mashtaka leo, Jumanne, Februari 12, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati wakiwasomea Maelezo ya Mashahidi na Vielelezo (Committal Proceedings).

Washtakiwa hao wamesomewa maelezo yao na jopo la  mawakili watano wa upande wa mashtaka wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Fredrick Manyanda akisaidiana na Tumaini Kwema, George Barasa, Ester Martin na Leonard Swai kutoka Takukuru.

Hatua hiyo ya kuwasomea Maelezo ya Mashahidi na vielelezo washtakiwa hao imehitimisha rasmi jukumu la Mahakama katika kesi hiyo ya Uhujumu uchumiambapo imefunga rasmi jalada la kesi hiyo na kuihamishia rasmi Mahakama Kuu, Kitengo Cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Kitilya na wenzake wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 58; ambapo mashtaka 49 kati ya hayo ni ya utakatishaji fedha, mashtaka matatu ya kughushi na mawili ya kutoa nyaraka za uwongo.

Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine ni Miss Tanzania wa 1996, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon, ambao walikuwa maofisa wa Benki ya Stanbic.

Wengine ni aliyekuwa kamishna wa sera na madeni wizara ya Fedha, Bedason Shallanda (kwa sasa yuko Ofisi ya Waziri Mkuu) na Alfred Misana ambaye alikuwa kamishna msaidizi wa sera na madeni kutoka wizara hiyo ambaye kwa sasa yuko wizara ya afya.

Mashtaka mengine yanayowakabili ni kungoza mtandao wa uhalifu, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu kula njama za kutenda kosa kwa nia ya kumdanganya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.

 

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti tofauti kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi.

Makosa hayo yalitokana na mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingireza, kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4, kupitia kampuni ya Egma T Ltd.

Katika mashtaka hayo wanadaiwa kujipatia Dola 6 milioni kwa njia za udanganyifu kupitia kampuni ya Enterprises Growth Market Advisors (Egma) kama ada ya uwezeshaji wa mkopo huo ya asilimia 2.4 na kisha kutakatisha kiasi hicho cha fedha.


Advertisement