Serikali yatangaza neema kwa wanunuzi wa korosho

Muktasari:

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amekaribisha kampuni na watu binafsi wenye nia ya kununua korosho kuwasilisha nia yao kwa katibu mkuu wizara ya viwanda na biashara.

Arusha. Wakati Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda akiwakaribisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kununua korosho ghafi tani 221,060, bado kitendawili cha kampuni ya Indo Power Solutions iliyoingia mkataba na Serikali kununua tani 100,000 hakijapata majibu.

Januari 30, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakati kampuni hiyo ikisaini mkataba wa ununuzi, mkurugenzi wa kampuni hiyo, Brian Mutembei alisema mara baada ya makubaliano hayo angefanya malipo na kuanza kubeba korosho.

Hata hivyo, baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya vilishangazwa na taarifa za kampuni hiyo kununua korosho yenye thamani ya Sh418 bilioni vikisema uwezo wake wa ukwasi ni mdogo.

Jana, akizungumza na wanahabari jijini Arusha, Waziri Kakunda alisema hadi juzi, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko chini ya timu ya pamoja ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo ilikuwa imekusanya jumla ya tani 221,060 za korosho ghafi kutoka kwa wakulima na imeweka kipaumbele kwa viwanda vya ndani ili kuviimarishia uwezo na kujenga mnyororo wa thamani.

Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akizungumza na Mwananchi alisema, “Bado (Indo Power Solutions) hajanunua, kuna mambo tunakamilisha.”

Alipoulizwa kuhusu taarifa kwamba kampuni hiyo ya Kenya haina uwezo wa kifedha wa kununua tani 100,000 za korosho, Waziri Kakunda alisema mnunuzi huyo anaendelea kukamilisha taratibu za kisheria na kibiashara na kwamba akishakamilisha atakabidhiwa shehena yake.

Hata hivyo, Kakunda alisema baada ya Serikali kujiridhisha, viwanda vya hapa nchini vitapata korosho ghafi ya kutosha na kujiandaa vizuri na msimu ujao wa uzalishaji huku akizikaribisha kampuni na watu binafsi wenye nia ya kununua zao hilo kuwasilishe nia yao kwa katibu mkuu wa wizara ya viwanda na biashara.

“Tukisema yeyote tunamaanisha awe mmiliki wa kiwanda, duka kubwa, wenye nia ya kusafirisha sehemu mbalimbali duniani au wenye nia ya kununua na kuzihifadhi ili baadaye wazibangue kwa utaratibu wowote watakaoona unafaa kwa matumizi ya kibiashara tunawakaribisha,” alisema Kakunda

Alisema Serikali inauza korosho kwa kiasi cha tani anazohitaji mnunuzi hata ikiwa ni 10 na kwamba jambo la msingi ni maelewano ya bei kwa kuzingatia kuwa Serikali imenunua korosho hizo kwa Sh3,300 kwa kilo kutoka kwa wakulima.

“Bei yetu tutakayoelewana lazima izingatie tumeinunua korosho hiyo kwa Sh3,300 kwa kilo, gharama za usafirishaji kutoka shambani hadi chama cha msingi, usafirisha kutoka chama cha msingi hadi ghalani, gharama za upakuaji na upakizi, kuhifadhi kwenye maghala, magunia, malipo ya vyama vya ushirika, tozo za kisheria za halmashauri na gharama za kuchangia elimu,” alisema Kakunda.