Serikali yatoa maelekezo matumizi rangi ya bendera ya Taifa, wimbo wa Taifa

Thursday December 13 2018
BENDERAPIC

Dar es Salaam. Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, imewaandikia barua wakuu wa vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na maendeleo ya jamii, vyuo vikuu na vishiriki na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuhusu matumizi sahihi ya rangi ya bendera na wimbo wa Taifa.

Katika barua hiyo iliyosambaa  katika mitandao mbalimbali ya kijamii inaeleza kuwa wizara hiyo imepokea maelekezo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, kuhusu matumizi sahihi ya vitu hivyo.

Maelekezo hayo yanabainisha kuwa kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi yanayofanywa na taasisi za Serikali.

“Kutokana na makosa hayo Wizara ya Mambo ya Ndani inaelekeza kuwa wimbo wa Taifa utapigwa kwenye dhifa za kitaifa, endapo hadhi ya sherehe haitambuliki, taasisi italazimika kuomba kibali kwa waziri mwenye dhamana,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

 

 

Advertisement

“Wimbo unatakiwa kuimbwa kwa ukamilifu beti zote mbili kwa kuzingatia ‘nota’ na maneno.”

 

Kuhusu rangi za bendera ya Taifa, barua hiyo inasema, “Rangi za bendera ya Taifa ni kijani, dhahabu, nyeusi  na bluu. Ni makosa kutumia rangi ya njano na uwiano wa bendera ni 2/3 katika urefu na upana.”

 

Mwananchi lilipozungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Leonard Akwilapo kupata ufafanuzi wa suala hilo amesema, “Unataka ufafanuzi wa gani? Kwani barua umeandikiwa wewe. Ungekuwa umelengwa wewe ningekupa ufafanuzi lakini sio. Walioandikiwa wanaelewa zaidi, sasa sijui unataka ufafanuzi gani.”

 

  


Advertisement