MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Shahidi aeleza alivyozika mwili na ulivyofukuliwa

Mmiliki wa Shule ya Sekondari Scolastica, Edward Shayo (aliyeinua chupa ya maji) baada ya kushuka kwenye gari la polisi eneo la Mahakama Kuu Kanda ya Mosh jana kusikiliza kesi inayomkabili ya mauaji ya mwanafunzi Humphrey Makundi aliyekuwa akisoma kidato cha pili shuleni hapo. Picha na Dionis Nyato.

Muktasari:

  • Kibwana alidai kazi ya kuuzika ilisimamiwa na polisi na ile ya kuufukua katika makaburi ya Karanga ilisimamiwa pia na polisi pamoja na madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Moshi. Mhudumu wa Manispaa ya Moshi, Samwel Tesha ameieleza Mahakama Kuu mjini Moshi namna alivyokabidhiwa mwili wa Humphrey Makundi, mwanafunzi wa shule ya Scolastica na kuuzika.

Tesha, ambaye ni shahidi wa saba wa mashtaka alidai jana kuwa mwili huo aliokabidhiwa kutoka Hospitali ya Mawenzi na kuuzika Novemba 12, 2017, ndio huohuo uliofukuliwa Novemba 17, mwaka huo.

Shahidi huyo alitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Firmin Matogolo akiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana. Alidai siku ya kuufukua mwili huo ulikuwa umeharibika na ulikuwa ukitoa harufu.

Alidai mahakamani hapo kuwa alikabidhiwa mwili huo kwa ajili ya kuuzika Novemba 12 ukiwa umeharibika na ulipofukuliwa, ulikuwa umeharibika zaidi.

Kibwana alidai kazi ya kuuzika ilisimamiwa na polisi na ile ya kuufukua katika makaburi ya Karanga ilisimamiwa pia na polisi pamoja na madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Mwili wa mtoto huyo uliokotwa na polisi Novemba 10 katika Mto Ghona mita 300 kutoka shuleni hapo. Ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Mawenzi na kuzikwa kwa madai kuwa haukutambuliwa.

Kesi hiyo inayovuta hisia za wakazi wengi wa ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro inamkabili mmiliki wa shule hiyo Edward Shayo, mwalimu wa nidhamu Labani Nabiswa na mlinzi Hamis Chacha.

Shahidi wa nane wa mashtaka, mkaguzi wa polisi Victor Frank alidai mahakamani hapo kuwa alisimamia uchukuaji wa sampuli katika mwili wa marehemu na kwa wazazi wake.

Akitoa ushahidi huku akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Joseph Pande, alidai katika uchunguzi wa mwili wa marehemu uliofanyika KCMC, ulibainika kuwa na jeraha kubwa kwenye fuvu.

Frank, ambaye ni mkuu wa idara ya uchunguzi wa maabara Mkoa wa Kilimanjaro alitaja sampuli zilizochukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa DNA kuwa ni pamoja na meno mawili ya Humphrey.

Pia alisimamia uchukuaji wa sampuli ya kipande cha nyama ya kwenye kalio na ya paja, cha mfupa wa paja na wa kifua, cha nyama ya kisigino na nywele sehemu za siri.

Shahidi huyo alidai kuwa katika uchukuaji huo wa sampuli pia walichukua sampuli za damu na mate ya baba wa marehemu, Jackson Makundi na mama yake, Joyce Jackson Makundi.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, sampuli hizo za baba na mama wa marehemu pamoja na viatu, mswaki na nguo za marehemu, walizichukua kutoka nyumbani kwa Jackson eneo la Komakundi, Marangu.

Shahidi huyo ambaye ni ofisa upelelezi alidai kwa siku tofauti aliwatuma maofisa wake kupeleka sampuli hizo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.

Baada ya ushahidi wake, jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa na Elikunda Kipoko, David Shillatu, Patrick Paul na Gwakisa Sambo walimhoji shahidi huyo na sehemu ya mahojiano hayo ni kama ifuatavyo:

Wakili Shilatu: Nitakuwa sahihi nikikwambia huu mwili uliofanyiwa DNA (vipimo vya vinasaba)ulikuwa ni wa hapa Moshi?

Shahidi: Tuliufukua kutoka makaburi ya hapa Moshi.

Wakili Sambo: Ulisema ulikuwa mochwari, katika upelelezi wako ni lini ulimfahamu Jackson Makundi?

Shahidi: Nilimfahamu tarehe 17.11.2017

Wakili Sambo: Ni kweli uliandika maelezo yako polisi?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Sambo: Mkiwa KCMC mochwari (chumba cha kuhifadhi maiti) Jackson Makundi alikuwepo?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Sambo: Unasema kuna raba ulipewa na Makundi, kweli siyo kweli?

Shahidi: Kweli

Kesi hiyo itaendelea leo