Shahidi kesi ya Zitto aeleza jinsi askari polisi, wananchi walivyouawa

Tuesday August 13 2019

Kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe

Kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe akizungumza na wakili Jebra KaKambole wakati wakitoka katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salam jana..Kulia ni Afisa mahusiano wa chama hicho Addo Shaibu. 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Kigoma (RCO), Mark Njela(45) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar Es Salaam nchini Tanzania kuwa mkaguzi wa Polisi, Ramadhani Mdimi na Koplo Mohamed Mzengo ni muongoni mwa watu wanne, waliuawa katika operesheni ya kuwaondoa wavamizi waliovamia eneo la Ranchi ya Taifa eneo la Burongole, iliyopo wilaya ya Uvinza mkoani humo.

Njela amesema hayo leo Jumanne Agosti 13, 2019, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi wakati akitoa ushahidi katika kesi ya uchochezi inayomkabili, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe.

Akiongozwa na wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka shahidi huyo alidai kuwa operesheni hiyo ilianza Oktoba 16, 2018 hadi  Oktoba 18, 2018 ilipositishwa, baada ya kutokea mapigano baina ya wavamizi wa eneo hilo na askari polisi.

Amedia SP Mdimi ambaye alikuwa kiongozi katika moja ya operesheni hiyo, aliuawa na wananchi hao  baada ya kuanguka chini wakati kikosi chake kilipokuwa kikirudi nyuma kwa ajili ya kujipanga upya.

“Mwanzo askari walikuwa wanatumia mabomu ya machozi kukabiliana na wavamiaji hao, lakini baadaye wavamizi hao walionekana kuwa na silaha za jadi huku wengine wakiwa na magobole na kuanza kulenga sehemu ambayo askari walipo.”

“Hali hiyo ilipelekea askari kutumia silaha za mto kwa ajili ya kujiokoa lakini wananchi wale walikuwa ni wengi hali  iliyopelekea askari kurudi nyuma kwa ajili ya kujipanga upya na kuhofia kuua watu wengi” amedia Shahidi huyo

Advertisement

“Wakati askari hao wakirudi nyuma, SP Mdimi alianguka chini na ndipo wananchi hao walipomshambulia na kumuua, pia walimuua Koplo Mohamed Mzego ambaye maiti yake ilikuja kupatikana kesho yake yaani Oktoba 18, 2018,” amedai.

Shahidi huyo aliwataja wananchi waliokufa katika operesheni hiyo ni Salum Deus ambaye alipigwa risasi na polisi wakati akijaribu kuwapiga risasi askari hao kwa kutumia silaha ya jadi aina ya Gobole na Gisena Mapembe.

Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumatano Agosti 14,2019 itakapoendelea.

Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo, Dar es Salaam.

Advertisement