Silinde: Maendeleo ya Tanzania hayategemei kukusanya kodi

Muktasari:

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde amesema kuboresha uwekezaji wa moja kwa moja na ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP) ndio msingi wa Taifa lolote duniani kupata maendeleo na si kukusanya kodi


Dodoma. Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde ameitaka Serikali ya Tanzania kutambua maendeleo ya nchi hayategemei kukusanya kodi.

Amesema maendeleo hutegemea kuboresha uwekezaji wa moja kwa moja na ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP).

Silinde ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 18, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

“Duniani kote maendeleo ya nchi hayategemei kodi pekee, nasema hivi kwa sababu wimbo humu ndani (bungeni) ni kodi tu. Nchi nyingi hutumia kodi kwa matumizi mengineyo na kulipa mishahara.”

“Dunia ya sasa kama unataka kuendelea kuna njia kubwa mbili, moja kuboresha uwekezaji wa moja kwa moja na ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP),” amesema Silinde.

Amebainisha katika bajeti ya wizara ya fedha imeanishwa miradi isiyotekelezeka na kutoa mfano mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambao hivi karibuni Rais John Magufuli alisema mwekezaji alikuwa na masharti magumu.

“Ukiacha mradi wa Bandari Bagamoyo kuna mradi wa Liganga na Mchuchuma, ujenzi wa reli ya kisasa za ule wa umeme katika mto rufiji. Miradi hii ingetumia mambo mawili niliyoyaeleza uchumi wa Tanzania ungekuwa katika hali gani?”

“Bandari ya Bagamoyo endapo tungeingia mkataba  ingekuwa Sh24 trilioni, Liganga na Mchuchuma Sh7 trilioni, reli ya kisasa Sh17 trilioni na ule wa umeme Sh6 trilioni.  Uchumi ungeongezeka kwa wakati mmoja kwa Sh124 trilioni. Leo pato letu la Taifa ni Sh125 trilioni (kwa sasa), fikiria hizi fedha zingeingia katika uchumi wetu, Serikali ingekuza pato la Taifa mara mbili zaidi,” amesema Silinde.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, Silinde amesema hata kama mkataba ulikuwa mbaya, si wote ingewezekana kukaa upya na kuurekebisha.

“Watu wangepata ajira katika maeneo hayo na fedha hizo zingeingia ndani na viwanda vingekuwa vingi. Bagamoyo kungekuwa na viwanda zaidi ya 1,000. Sasa sisi tunatumia fedha za ndani na kukopa kwenye mabenki kutekeleza miradi.”

“Mfano mradi wa SGR kwa jinsi unavyotekelezwa Magufuli anaweza kutoka madarakani mradi haujakamilika, ule wa umeme bado haujaanza. Tunakwenda lakini ni mwendo wa konokono,” amesema Silinde.

Ameongeza, “Wabunge tunashauri lakini maneno yetu hayamfikii Rais. Juzi tu hapa wakati Rais anazungumza na wafanyabiashara kuna mambo yalizungumzwa na wafanyabiashara hivi humu ndani hatujawahi kuyasema?”

“Mwaka 2006 nikiwa UDSM (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), Mbeki (Thabo-Rais mstaafu wa Afrika Kusini) alifanya mdahalo akasema kazi ya urais itakuwa ngumu kama una washauri wabovu na nzuri kama una washauri wazuri.”

Amesema hivi sasa mtaani Rais Magufuli analalamika kuwa urais mgumu, “Kumbe jibu ambalo Mbeki alituambia mwaka 2006 leo naliona, amezungukwa na washauri wabovu ndio maana anaona kazi ngumu ndio maana anakutana na wafugaji, wafanyabiashara, wachimbaji wadogo wa madini, yaani anafanya kila kitu Bunge tunafanya kazi gani?”

Silinde ambaye ni mjumbe wa kamati ya bajeti amesema mwaka 2018 kamati hiyo ilikuja na mapendekezo 11 lakini Serikali ikayakataa na baadaye kuja na mapendekezo ya mabadiliko ya mambo mbalimbali, yakiwemo iliyoyakataa.

Pia, aligusia ukuaji wa viwanda akisema ni ngumu kufikia malengo kutokana na kutokuwa na malighafi.

“Tunakwenda kwenye sera ya viwanda wakati hakuna malighafi, unazalisha kiwanda wakati huna pamba, tumbaku uzalishaji umeshuka, korosho nayo imeshuka. Sasa unaanzisha kiwanda kwa malighafi ipi,” amehoji Silinde.