Sumaye, Mahanga wazungumzia hatima yao Chadema

Moshi. Marafiki wa Edward Lowassa ambao walihamia naye Chadema wakati wa wimbi la Uchaguzi Mkuu 2015, wamegoma kufuata mkumbo mwingine kurejea CCM kama alivyofanya waziri huyo mkuu wa zamani Ijumaa iliyopita.

Miongoni mwao ni Frederick Sumaye, aliyekuwa waziri mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, ambaye aliondoka CCM wakati wa wimbi hilo na baadaye kujiunga na Chadema na Dk makongoro Mahanga, ambaye alikuwa mbunge kwa miaka 14 na naibu waziri wa kazi.

Sumaye, mmoja wa wazungumzaji waliovuta hisia za wengi katika kampeni za mwaka 2015, aliiambia Mwananchi jana kuwa hana mpango wa kuondoka Chadema kwa vile lengo lililompeleka halijatimia na Watanzania hawatamuelewa, wakati Dk Mahanga, amesema hana tena sababu za kumfuata CCM.

Lowassa, mmoja wa makada waliokuwa wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa na CCM kugombea urais, alikatwa jina lake na Kamati ya Maadili na baadaye alihamia Chadema ambako alipewa fursa ya kutimiza ndoto ya kuwania urais aliyoiita “Safari ya Matumaini”.

Mwanasiasa huyo alifuatwa na wanachama wa kada mbalimbali, wakiwamo wenyeviti wa mikoa, wabunge, madiwani na wenyeviti wa kata.

Ijumaa iliyopita, Lowassa aliongozana na mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz kwenda ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam kutangaza uamuzi wake wa “kurudi nyumbani”.

‘Lowassa alionewa CCM’

Lakini Dk Mahanga amesema alimfuata Lowassa wakati ule kwa sababu aliona ameonewa na chama na kwa sasa hajaondoka Chadema kwa sababu ya kuonewa.

“Kulikuwa na mambo ya ajabu sana ndani ya chama. Kwa ile huruma na ikizingatiwa amekuwa rafiki yangu kwa miaka 30, iliniuma sana,” alisema.

“Tukaamua kwa pamoja jioni ile tuhame. Safari hii sioni kama ameonewa. Sioni ugomvi wowote na Kamati Kuu ya Chadema, sasa nitakwenda tu CCM kwa sababu ya jina? “Ninamuonea huruma mwenyekiti (Freeman) Mbowe ambaye yuko gerezani na Tundu Lissu ambaye anatembea na magongo huko Ulaya.”

Sumaye aja na mpya

Akizungumzia hatua hiyo, Sumaye, aliyekuwa waziri mkuu kwa miaka 10, alisema hakumfuata Lowassa Chadema na kwamba mwanasiasa huyo hakuhama na wanachama wengi kama inavyoaminika.

“Nilikwenda kwa sababu ya kutaka kuimarisha upinzani ili kujenga demokrasia ya kweli nchini. Lowassa alikuja na watu kama 10 hivi au zaidi sina takwimu,” alisema Sumaye.

Alisema walienda Chadema sababu waliona kimeshakuwa chama kikubwa na ndio maana kiliongeza idadi ya kura.