TBS yataja sababu kufanya ukaguzi bidhaa za Afrika Mashariki

Thursday August 1 2019Ofisa masoko mwandamizi wa TBS, Gladness Kaseka

Ofisa masoko mwandamizi wa TBS, Gladness Kaseka 

By Filbert Rweyemamu, Mwananchi [email protected]

Arusha. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema utaratibu wa kuchunguza bidhaa zilizopatiwa vyeti vya uchunguzi  katika nchi za Afrika Mashariki(EAC) ni wa kawaida katika kulinda afya za watumiaji.

Ofisa masoko mwandamizi wa TBS, Gladness Kaseka amesema hayo leo Alhamisi Agosti Mosi, 2019 katika Maonyesho ya Nanenane.

“Sheria za ubora wa viwango katika nchi za EAC zimeoanishwa kwa lengo la kuwezesha biashara kufanyika kwa haraka zaidi na kila nchi inaheshimu viwango vya uchunguzi katika maabara husika.”

“Bidhaa ikishapewa cheti cha ukaguzi kinachofanyika ni kujiridhisha ubora wake ambao hauchukui muda mrefu,” amesema Kaseka.

Naye ofisa mkaguzi wa TBS kanda ya Kaskazini, January Faustine amesema wanashiriki maonesho hayo ili kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia matumizi ya bidhaa zenye ubora ambao wao wana jukumu la kusimamia viwango.

Amebainisha kuwa wameendesha ukaguzi kwenye masoko ya nguo za mitumba katika miji ya Arusha na Moshi ambako walifanikiwa kupata nguzo za ndani zenye ubora hafifu zinazoweza kusababisha madhara ya kiafya kwa watumiaji.

Advertisement

Katibu tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega amesema maonyesho ya 2019  yatalenga kuwapa elimu makundi ya wananchi kutoka Mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha kujifunza mbinu mbalimbali za kuongeza tija katika shughuli zao.

 

Advertisement