Tanzania yazidi kuporomoka uhuru wa habari

Dar es Salaam. Tanzania imeshuka kwenye viwango vya uhuru wa habari kutoka nafasi ya 93 mwaka jana hadi nafasi ya 118 kati ya nchi 180 duniani kote mwaka huu kwa mujibu wa ripoti ya 2019 World Press Freedom Index.

Huu ni mwaka wa tatu mfululizo ambapo Tanzania imekuwa ikishuka kwenye viwango hivyo ambapo mwaka 2017 ilikuwa nafasi ya 83, hivyo kuifanya kuanguka nafasi 25 mpaka mwaka huu.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas ameipuuza ripoti hiyo akisema Serikali inajua inachokifanya kwa taifa.

“Kwanza kama Serikali hatujashangazwa na ripoti hiyo kwa sababu tunajua nini tunakifanya kwa faida ya Tanzania ya leo na kesho.”

“Huwezi kupima uhuru wa habari kwa kuorodhesha matukio ambayo yanajitokeza katika jamii na siyo yanayotendwa na Serikali kama la Azory (Gwanda),” alisema Dk Abbas na kuongeza:

“Huwezi kupima uhuru wa habari eti kwa kuangalia kuna waandishi wa CPJ walikuja Tanzania licha ya kukiuka sheria na taratibu za nchi wanapokamatwa unasema unakiuka uhuru wa habari.”

“Hili tutalifanya bila kujali ripoti gani ina mtazamo gani kwetu, kwetu sisi tuna jukumu la kikatiba kufanya hivyo.” a

Akizungumzia ripoti hiyo, Katibu mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema ripoti hiyo inaakisi hali halisi ilivyo nchini.

“Hiyo inaonyesha hali halisi iliyopo katika nchi yetu. Mazingira ya sasa hatujawahi kuyaona, hata katika mfumo wa ukiritimba wa kisiasa hatukuwa na matatizo ya uhuru wa habari kama tuliyonayo sasa.”

“Pia hatuijawahi kuwa na waandishi wanaopotea na hatujui kinachofanyika. Waandishi wanapigwa, wanatiwa ndani kinyume cha sheria na kumekuwa na tishio kwa uhuru wa wahariri kwa kuingiliwa na mamlaka za Serikali,” alisema.

Waziri kivuli wa Habari, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu alisema hali ya uhuru wa habari imekuwa mbaya kuliko wakati wowote tangu Tanzania ipate uhuru. “Hii ripoti inaakisi hali iliyopo nchini ndiyo maana hotuba yangu imezuiliwa bungeni kwa kunyofolewa asilimia 80 ya maoni yetu.

Juzi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alitaja wingi wa vyombo vya habari kama kigezo cha kuongezeka kwa uhuru wa habari nchini alipokuwa akisoma hotuba ya makadirio na matumizi ya mwaka 2019/20 Bungeni Dodoma na kukosolewa na wadau mbalimbali wa habari wakisema uhuru wa habari haupimwi kwa wingi wa vyombo vya habari.