MAWAIDHA YA IJUMAA: Tuzitathmini swaumu zetu katika mambo matano

Mwezi mtukufu wa Ramadhani ndio huu ambao kwa leo tayari tumo katika kumi la pili, ambalo ni maarufu kwa jina la ‘kumi la Maghfirah’ yaani kusamehewa dhambi.

Sio vyema kuendelea kufunga bila ya kujitathmini na kuitathmini swaumu yenyewe ili kabla ya mwezi haujamalizika wote, kila mfungaji ajijue iwapo amenufaika au amepata hasara.

Ukweli ni kwamba ‘atakayezembea’ na mwezi ukaisha bila ya kunufaika nao kwa kuyapata yaliyoahidiwa kupatikana ndani ya mwezi huu, huyo amepata hasara ambayo haoisahau katika historia ya maisha yake.

Ili kujitathmini ni vyema kila mmoja wetu ayatafakari mambo matano kwani siku kumi tulizomaliza kufunga zinatosha kupata kipimo kwamba tunatakiwa kuongeza kufanya mema na kurekebisha kasoro zilizojitokeza.

Jambo la kwanza: Swaumu inatakiwa imletee mfungaji uchamungu. Uchamungu maana yake ni sifa anayokuwa nayo mtu ambayo inamfanya apate ‘msukumo’ maalum wa kufuata maamrisho yote Muumba na kuacha makatazo yake. Mchamungu huwa anajiepusha na mabaya na anajiweka karibu na kuyafanya yaliyo mema yanayomridhisha Mola wake na wanaadamu wenzake.

Kama mfungaji amefunga siku kumi na bado katika nafsi yake ‘anazitamani’ dhambi, huyo bado swaumu yake ina kasoro na ndio maana haijamtibu katika ugonjwa wa kutenda dhambi.

Haya mfungaji mwenzangu hebu sasa jipime: Je moyo wako unatamani dhambi ambazo uliteleza na kuzifanya kabla ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani au moyo wako unajutia kwa dhambi hizo?

Bado siku za kujirekebisha zipo ili kama bado hujabadilika hicho ndio kipimo tosha kwamba swaumu yako ina kasoro nyingi na ndio maana haikupi matokeo mema. Jirekebishe katika siku zilizosalia.

Mwenyezi Mungu amesema katika Quran Tukufu: “Enyi Waumini mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili muwe wacha-Mungu”.

Sasa jipime mfungaji kwa siku kumi hizi, Je ushaanza kujihisi kumcha Mwenyezi Mungu?

Jambo la pili: Swaumu inatakiwa imletee mfungaji zawadi ya kusamehewa madhambi. Ili mfungaji ujijue kama umesamehewa madhambi au laa ni lazima kujiuliza iwapo wakati unamuomba Mwenyezi Mungu msamaha, ulikdihi vigezo vya kuomba msamaha?

Kama umekidhi vigezo, jua umesamehewa. Na kama hujakidhi jua kwamba hujasamehewa hata kama umeomba msamaha mara elfu moja.

Mfungaji anatakiwa akifunga afuate sheria za swaumu ambazo ni kufunga kula, kunywa na hitajio la kimwili. Lakini pia mdomo wake afunge asitukane na asiseme lolote baya, masikio yake ayafunge asisikilize mambo yaliyokatazwa na sheria na macho yake ayafunge yasiangalie yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu.

Swaumu inayofungwa kwa namna hiyo yenyewe inafuta madhambi ya mfungaji. Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Yeyote mwenye kuifunga Ramadhani na akajua mipaka ya Ramadhani na akajilinda na yale ambayo mfungaji anatakiwa kujilinda nayo Ramadhani itamfutia madhambi yote yaliyokuwa kabla ya Ramadhani”.

Wakati wa kutamka kuomba msamaha, muombaji msamaha wa kweli anatakiwa azingatie mambo matatu: ajutie dhambi zake, ajivue na dhambi hizo na asiwemo ndani yake wakati anaomba msamaha, na amuahidi Mwenyezi Mungu kwamba hatorudia tena kufanya dhambi hizo. Kama mfungaji anayeomba msamaha amezingatia hayo kwa hakika huyo amesamehewa.

Jambo la tatu: Swaumu inatakiwa imletee mfungaji tabia njema. Mfungaji anatakiwa awe na tabia njema hasa ya kujizuia kuleta madhara yoyote kwa jamii na ndio maana anafundishwa kwamba iwapo atatokea mtu akamkera kwa lolote kwa kumtukana au kwa kumfanyia ujinga wowote, yeye anatakiwa aseme kimoyomoyo kwamba “Innii Swaaim” (hakika mimi nimefunga).

Jambo la nne: Swaumu inatakiwa imletee mfungaji ukarimu. Ukarimu ni ile sifa ambayo mwanaadamu akiwa na kitu anawaonea huruma wengine ambao hawana, hivyo anapenda kugawana nao.

Mtu yeyote ambaye anafunga lakini sifa ya ukarimu hana, anatakiwa ajue kwamba swaumu yake bado haijawa na thamani. Muislamu anatakiwa ajue kwamba aya ya Quran Tukufu iliyozungumzia swaumu imewataja waumini na waumini wa kweli miongoni mwa sifa zao ni ukarimu.

Bwana Mtume Muhammad (Swallallaahu Alayhi Wasallam) amesema: “Mambo mawili hayakutani kwa muumini, ubakhili na tabia mbaya”. Hivyo basi mfungaji anatakiwa ajipime na ajitathmini juu ya ukarimu na asiwe bakhili. Na huo ukarimu wenyewe uwe ni mpana kuanzia kwa familia yake, majirani zake, mayatima, wajane, walemavu, kwa ndugu zake na kwa wenye shida mbalimbali wanaoomba na wasioomba. Mfungaji bakhili bado hajafaidika na swaumu yake.

Jambo la tano: Swaumu inatakiwa imletee mfungaji afya njema. Mfungaji anatakiwa afaidike na swaumu yake kwa kupata afya njema, kwani maradhi mengi ya mwanaadamu yanatokana na kula bila mpangilio.

Maagizo ya kula kwa mpangilio ni mwanaadamu kuligawa tumbo lake katika theluthi tatu: theluthi ya chakula, theluthi ya maji na theluthi ya pumzi. Hivyo mfungaji asizimalize theluthi zote kwa kula sana wakati wa kufuturu au wakati wa daku.

Ni vyema wafungaji wakaelewa kwamba futari lengo lake sio kulipizia vyakula vyote vilivyokosekana mchana na daku lengo lake sio kujikinga na njaa ya swaumu. Hivyo ili tufaidike na swaumu zetu tujipime na tujitathmini katika mambo hayo matano.

Mwandishi wa makala haya ni mwenyekiti wa Arrisaalah Islamic Foundation.

0754 299 749/0 784 299 749