UTAWALA BORA: Wapinzani bungeni waijengea hoja tume huru ya uchaguzi

Dodoma. Wiki ilimalizika kwa Bunge kujadili hotuba mbili za bajeti--Tamisemi na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), lakini wabunge wa upinzani waliegemea zaidi kwa Waziri George Mkuchika.

Walishikilia hoja ya kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ili kuweka mazingira ya usawa, ikiwa ni moja kati ya mambo sita yaliyojitokeza kwenye mjadala huo.

Katika mjadala wa bajeti hizo, kila wabunge wawili wa upinzani waliposimama kuchangia, mmoja kama si wote alidai tume huru ya uchaguzi.

Baadhi walionyesha umuhimu wa tume hiyo kwa kutoa mfano jinsi mawakala wa upinzani wanavyozuiwa kuingia vituoni wakati wa chaguzi ndogo na madai kuwa wasimamizi wa uchaguzi hutangaza watu ambao hawakushinda pamoja na hoja ya masanduku ya kura kuibwa.

Wakati wabunge wa upinzani wakilia na tume huru, wenzao wa CCM waliwajibu kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyopo sasa ni huru.

Mengine yaliyotikisa ni haja ya madiwani kuongezewa posho, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kutokuwa na fedha za kutosha na hivyo kushindwa kukamilisha miradi kwa wakati, Serikali kumaliza ujenzi wa majengo ya shule, vituo vya afya na hospitali.

Mengine ni vitendo vya wakuu wa mikoa na wilaya, wafungwa kurundikana magerezani kwa kesi zenye dhamana, uhaba wa watumishi katika sekta ya afya na elimu.

Suala la tume huru ndio lilitamalaki, huku wabunge wakitaka sheria ifanyiwe marekebisho ili kuondoa hali ya sintofahamu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Suala hilo lilianzia katika maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2019/2020, ambayo ilitaka Serikali ipeleke muswada wa marekebisho ya Katiba kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuwezesha kuundwa kwa tume huru.

Kambi hiyo inataka mamlaka ya Rais ya kumteua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wengine au wakurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi yaondolewe na badala yake wateuliwe kwa utaratibu mwingine utakaowekwa na sheria hiyo.

Pia, kuanzishwa kwa mfuko wa fedha wa tume hiyo, jambo litakalohakikisha uwepo wa fedha za kuendesha shughuli za uchaguzi nchini wakati wote bila kutegemea huruma ya Serikali. Na tatu ni kuondoa katazo la kuishtaki au kupinga uamuzi wa tume mahakamani kuhusu uendeshaji wa uchaguzi.

“Mkurugenzi atakayetangaza mpinzani kushinda atakiona cha mtema kuni, alisema mbunge wa Tarime Mjini, John Heche kwa maelezo kuwa hayo ndio maagizo ya Rais John Magufuli.

“Kwa uzoefu wa chaguzi zilizofanyika huko nyuma hatukuwahi kuona uporaji wa matokeo ya uchaguzi yakifanyika wazi kama sasa. Hivi sasa ni kawaida mnaweza kukusanya matokeo yenu na mkaona mmeshinda ila msimamizi wa uchaguzi anataka mshindi mwingine.

“Hivi sasa wapigakura wanaweza kuwa wengi kuliko waliojiandikisha. Mawakala wanazuiwa vituoni. Haya mambo yanaweza kufanyika katika chaguzi ndogo ila uchaguzi mkuu yakifanyika hali itakuwa mbaya sana.

“Suluhisho ni kuleta mabadiliko ya Katiba bungeni ili turekebishe kifungu kuhusu tume ya uchaguzi ili twende katika uchaguzi kwa amani,” alisema Heche.

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, alisema “mtu yeyote anayekataa kufanya jambo jema ujue ni muovu. Kama hawaibi katika uchaguzi kwa nini hawataki kuondoa shari, tufanye mchakato wa kuwa na tume ambayo kila mtu akishindwa kunakuwa hakuna malalamiko”.

“Inatakiwa iwepo tume huru ambayo mfumo wa uundwaji wake tutautengeneza sisi, mfano tume inaweza kuwa na wawakilishi kutoka kila chama,” alisema.

Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali alisema: “Nina mashaka na uadilifu wa watu waliopo katika tume maana kwa sasa wanabishana hadharani tena kwa mrengo wa upande mmoja. Namna tume inavyoundwa inapendelea chama kilichopo madarakani.”

Lakini mbunge wa Mtera (CCM) Livingston Lusinde alisema ni kawaida kwa wabunge wa upinzani kuanza kuweweseka kila inapofika kipindi ya uchaguzi lakini hawana hoja.