Ujerumani yamuahidi Magufuli kiwanda kikubwa

Muktasari:

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman J.A. Al Thani Ikulu jijini Dar es Salaam na kutumia fursa hiyo kukaribisha uwekezaji kutoka nchi hiyo.

Dar es Salaam. Kutokana na uhakika wa gesi ya Mtwara kutoa malighafi, jana Kansela wa Ujerumani, Angela Markel amempigia simu Rais John Magufuli na kuahidi kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea ili kuendeleza kilimo nchini.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema, Markel alipiga simu juzi na kuzungumza na Rais Magufuli mambo kadhaa yanayohusu diplomasia ya mataifa haya mawili huku akiweka msisitizo kwenye sekta ya kilimo.

Katika mazungumzo hayo, Markel alimweleza Rais Magufuli nia ya Ujerumani kuwaleta wafanyabiashara watakaowekeza katika sekta tofauti za uchumi ikiwamo kujenga kiwanda hicho kitakachokuwa kikubwa kuliko vyote Afrika.

Hazina ya zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 za gesi asilia imegundulika nchini ambayo licha ya kuzalisha umeme wa kutosha na matumizi mengine, inatoa malighafi muhimu za uzalishaji wa mbolea za viwandani.

Katika mazungumzo yao, Kansela Markel alimwalika Rais Magufuli kwa mara ya pili kutembelea Ujerumani, ziara itakayotanguliwa na mikutano ya mawaziri wa Tanzania na Ujerumani.

Markel alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi za kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji, kupambana na rushwa na kuimarisha miundombinu.

Rais Magufuli alimshukuru Markel kwa dhamira yake ya kukuza uhusiano na akamueleza kuwa Tanzania itahakikisha inajenga mazingira mazuri ya ushirikiano, biashara na uwekezaji.

Alimpongeza Markel kwa uongozi wa zaidi ya miaka 13 ya kuwatumikia Wajerumani na akamhakikishia kudumisha ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.

Oktoba 2016, kampuni ya Helm AG kutoka Ujerumani iliahidi kujenga kiwanda cha mbolea chenye thamani ya Dola1.5 bilioni za Marekani mkoani Lindi. Kitakapokamilika na kuanza uzalishaji, ilielezwa kiwanda hicho kitazalisha tani 3,900 za urea na 2,200 za ammonia kila siku.

Kufanikisha ujenzi huo utakaotoa ajira zaidi ya 3,500 za moja kwa moja, ilielezwa kuwa wadau kadhaa watakuwa na hisa. Wadau hao ni kampuni ya Haldor Topsoe AS ya Denmark, Ferrostaal Industrial Projects ya Ujerumani na Fauji ya Pakistan kwa ubia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Alipoulizwa kuhusu maendeleo ya mradi huo, kaimu mkurugenzi mkuu wa TPDC, Kapuulya Musomba alisema kwa sasa wanakubaliana bei ya gesi. “Mambo mengine yamekamilika, tukikubaliana kwenye bei ya gesi, ujenzi utaanza mara moja,” alisema.

Magufuli akutana na kiongozi wa Qatar

Jana, Rais Magufuli alikutana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, Rais Magufuli aliwakaribisha wananchi kutoka Taifa hilo la Kiarabu kuwekeza kwenye usindikaji wa gesi, madini, utalii na usafiri wa anga.

“Natambua Qatar mna utaalamu wa kuchakata gesi na sisi tunayo nyingi, kwa hivyo nawakaribisha mje tushirikiane kuwekeza. Natambua nyie ni wanunuzi wakubwa wa dhahabu, sisi tunayo nyingi na hivi sasa tumeanzisha vituo vya ununuzi, nawakaribisha na tutawapa ushirikiano wote mtakaouhitaji,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia aliiomba Qatar kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo uzalishaji wa umeme, ujenzi wa reli, barabara na madaraja. Pia, amemualika Mtawala wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kufanya ziara hapa nchini.

Sheikh Mohammed alimshukuru Rais Magufuli na Serikali yake kwa kuendelea kushirikiana na Qatar katika masuala mbalimbali na kusisitiza kuwa nchi yake inathamini uhusiano huo.

Alisema Qatar ipo tayari kufanyia kazi maombi yaliyotolewa na Rais Magufuli ikiwamo kuzileta kampuni za nchi hiyo kuja kuwekeza katika maeneo yenye fursa zenye manufaa kwa pande zote mbili.

Mazungumzo ya viongozi hao yalihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba, Balozi wa Tanzania nchini Qatar Fatma Rajab na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Abdullah Jassim Mohammed Al Medadi.