Ujumbe wa Nyalandu kwa Chadema

Muktasari:

Mbunge wa zamani wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye kwa sasa ni mwanachama wa Chadema amekiomba chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania kujifunza kwenye vyama vikongwe vya zamani ili kiweze kuaminiwa na kushika uongozi wa nchi, akitaka uwepo mfumo wa wazi wa kidemokrasia  wa kupata wagombea wake

Arusha. Mbunge wa zamani wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amesema ili Chadema inaminiwe, inapaswa kujifunza kwenye vyama vikongwe vya zamani kwa lengo la kushika uongozi wa nchi wakati huu kikiwa chama kikuu cha upinzani nchini.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi alisema ni muhimu kila mwanachama kutamani uwepo mfumo wa wazi na kidemokrasia ambao unatoa fursa kwa chama kuwapata wagombea wake katika ngazi mbalimbali.

“Kwa sasa hivi sio suala la nani atakua nani, nadhani jambo la msingi uwekwe mfumo ulio wazi ambao pia ni wa kidemokrasia wa kuwapata wagombea katika ngazi zote. Nafasi ya urais ni muhimu kwa wanachama wanaotaka kuwania kuwafikia wapigakura maeneo yote nchini ili mgombea anayeshinda kwenye kura za maoni awe na nafasi kubwa ya kupambana na mgombea wa CCM,” alisema Nyalandu.

Alisema utaratibu huo utafanikiwa kwa sababu sasa hivi Chadema inatekeleza mkakati wake wa Chadema Msingi, mfumo wa kuwashirikisha wafuasi na mashabiki wa chama hicho kuanzia ngazi ya mashina hadi ngazi ya juu unaolenga kuwafanya wanachama kutambuana na kuelewa misingi ya chama.

Nyalandu alisema mfumo wa kura za maoni kwa njia ya uwazi unaondoa mashaka na manung’uniko kwa wanachama kwa mgombea aliyepita na wanakua tayari kumpigania kwenye uchaguzi unaojumuisha vyama vingine wakijua aliyepita kwenye kura za maoni alipita kwa njia ya uwazi na kidemokrasia.

“Chama chetu sasa kijiandae kuweka huo mfumo ambao utakua na masharti yanayoeleza namna gani kinyang’anyiro cha wagombea urais wote ndani ya chama utakuwa, ni muhimu kila mwanachama mwenye nia apate fursa ya kufahamika. Namini utaratibu huu utapanua wigo kwenye mikutano ya maamuzi,” alisema Nyalandu.

Alisema wananchi wengi wanayo imani na Chadema na ndio maana ukuaji wake upo wazi kwa kuangalia kwenye chaguzi zilizopita ambako alisema imekua ikiaminiwa kwa kuongeza viti katika ngazi ya Serikali za Mitaa, madiwani, majimbo ya ubunge na hata kura za wagombea urais ikilinganishwa na chaguzi zilizotangulia.

Hajutii kuhama CCM

Kada huyo wa zamani wa CCM ambaye mwaka 2015 alikuwa miongoni mwa walioomba ridhaa ya kuwania urais kabla ya kubwagwa kwenye kura za maoni alisema hajutii kukihama chama hicho kwa sababu Chadema kinatoa fursa ya kushirikiana na wananchi kupigania demokrasia.

Aliongeza kuwa kabla ya kuondoka CCM, alitafakari kwa kina kwa miaka miwili na alipochukua uamuzi ulikua thabiti na ataendelea kuuamini kwa ajili ya kufikia Tanzania inayotoa fursa pana kwa kila mwananchi katika kupigania demokrasia.

Alisema shauku yake ni kuona nchi ambayo hakuna mtu anayebaguliwa kwa sababu za imani ya kisiasa, kidini, kikabila au namna nyingine yoyote na kuachia kizazi kijacho kikiwa katika hali ya furaha na kupendana.

Waliohama Chadema

Kuhusu viongozi wa ngazi mbalimbali walijitoa Chadema na kujiunga CCM kwa madai kwamba chama hicho cha upinzani kimekosa mwelekeo, alisema hawezi kuwazungumzia waliondoka kwa sababu walionyesha uhuru wao kama yeye alivyofanya lakini anakiona Chadema kama chama kikuu cha upinzani nchini chenye viongozi madhubuti na wenye nia ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.

Nyalandu alisema hakujiunga Chadema kupinga kila kitu cha Serikali au kuiua CCM au kuiua Chadema, bali kuwa na mawazo mbadala yaliyopo Chadema yenye kujenga nchi na kuimarisha mshikamano wa watu wote bila kujali tofauti zao.

Kugombea urais 2020

Kuhusu iwapo atagombea urais kama, Nyalandu ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa ikiwamo waziri wa Maliasili na Utalii alisema jambo la msingi kwa sasa ni chama chake kuweka utaratibu wa wazi na kidemokrasia ambao kila mwanachama ataweza kuutumia kuwania nafasi anayopenda.

“Chadema inapaswa kuweka mfumo wenye kuonyesha utaratibu mahsusi ambao upo wazi kabisa na wa kidemokrasia. Nashauri hadi mwezi Juni mwaka huu uwe umekamilika kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu 2020,” alisema Nyalandu.