Umoja wa Ulaya kuimarisha mazingira ya uwekezaji SADC

Wednesday August 7 2019

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika(SADC) wamezindua programu ya miaka mitano kusaidia uimarishaji wa mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara katika nchi 16 za jumuiya hiyo.

Uzinduzi huo unafanyika wakati Mkakati wa Viwanda wa SADC ukiweka dhamira ya kuongeza kasi ya kuimarisha ushirikiano na ushindani  wa kiuchumi kutoka katika nchi zisizokuwa wanachama wa SADC.

Programu hiyo ilizinduliwa jana Jumanne Agosti 6, 2019 Jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ya pili ya maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda kwa nchi 16 za SADC. Jumla ya washiriki 3,001 wakiwamo wafanyabiashara wenye manada 172 kutoka nje ya Tanzania.    

Maonyesho hayo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2016 nchini Eswatini, mwaka 2017 nchini Afrika Kusini , mwaka 2017 nchini Namibia na awamu ya nne mwaka huu nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya kwanza 2015/30 ya Mkakati wa Viwanda wa SADC 2015/2063.

Programu hiyo itatekelezwa kwa bajeti ya euro 14 milioni, sawa na Sh35 bilioni chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Ulaya (EDF). Programu hiyo itakuwa sehemu ya programu zenye thamani ya euro 70 milioni, sawa na takribani Sh175 bilioni.

Akizungumza katika uzinduzi wa programu hiyo, Katibu Mtendaji wa SADC, Dk Stergomena Tax alisema matokeo ya ushirikiano kupitia programu hiyo yatachochea mazingira mazuri ya biashara, kupanua mtandao wa biashara ndani ya jumuiya hiyo hatua itakayokuza soko la ajira.

Advertisement

“Lakini itasaidia kuchochea ukuaji wa miundombinu ndani ya SADC na kuwezesha nchi wanachama kuongeza ushiriki katika mtangamano huo pamoja na ushindani katika mnyonyoro wa thamani,” alisema.

Mkuu wa Kitengo cha uwekezaji na ubunifu katika umoja huo, Kay Parplies alisema ushirikiano wa Afrika na umoja huo unahamasisha uwekezaji, maendeleo endelevu na kukuza ajira.

“Programu hii madhubuti ni mfano unaodhihirisha mahusiano yaliyopo na tunaamini tutaendeleza kuimarisha mahusiano hayo,” alisema

Advertisement