Upelelezi kesi ya waliotapeli kwa kutumia jina la mke wa Rais Magufuli haujakamilika

Muktasari:

  • Upelelezi wa kesi ya kujipatia Sh4.487 milioni kwa kutumia jina la Janet, mke wa Rais John Magufuli inayowakabili washtakiwa wanne haujakamilika

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kujipatia Sh4.487 milioni kwa kutumia jina la Janet, mke wa Rais John Magufuli inayowakabili washtakiwa wanne haujakamilika.

Washtakiwa katika kesi hiyo ambao ni ndugu wa familia moja ni Saada Uledi, Maftaa Shaaban, Heshima Ally na Shamba Mdaila.

Wakili wa Serikali Glory Mwenda amedai leo Alhamisi Mei 16, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde, kuwa upelelezi wa kesi hilo haujakamilika na kuomba  tarehe nyingine.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne ikiwamo kula njama na kutenda kosa kwa kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa facebook.

Inadaiwa kati ya Januari 2017 hadi Machi 2019  jijini Dar es Salaam, walifungua akaunti ya  Facebook yenye jina la Janeth Magufuli na kuchapisha taarifa ya uongo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa, Janeth amefungua taasisi ya kutoa mikopo kwa watu na moja ya sharti la mkopo huo ni kutuma fedha kwanza kama kinga ya mkopo atakaopewa mhusika wakijua ni uongo.

Katika shtaka lingine, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kupitia taarifa hiyo ya uongo na kwa nia ovu, walijipatia Sh4,487,000 ambazo zilitumwa kwa njia ya simu kupitia kwa Paul Kunambi.

Pia, washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha ambazo ni Sh4,487,000 huku wakijua zilitokana na kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 30, 2019 itakapotajwa tena na washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana.