Utouh awashauri wasioridhika na CAG waende mahakamani

Tuesday April 30 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh amewashauri watu wanaokosoa au kupinga ripoti zinazotolewa na ofisi hiyo kwenda Mahakama Kuu kushtaki, akisema hivyo ndivyo Katiba na sheria zinavyoelekeza.

Utouh amesema utaratibu wa kukosoa ripoti za CAG upo kwenye sheria na Katiba.

“Mahakama Kuu ndiyo itachunguza kuona kama ukaguzi wa CAG na conclusive (ukamilifu) wake umefanywa kwa utaratibu unaokubalika,” alisema.

Suala la mawaziri kujibu ripoti ya CAG limechukua sura mpya hivi karibuni baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kumwita CAG ni mwongo alipokuwa akijibu hoja za wabunge bungeni jijini Dodoma.

“Sijawahi kuona mtu mwongo kama CAG katika nchi ya Tanzania. Haiwezekani, sare zinazodaiwa kuwa hewa… mimi waziri ambaye nimwekwenda kwenye makontena na magodauni ya Polisi na nimekuta sare, halafu CAG anapeleka taarifa kwa Mheshimiwa Rais ya uongo kwamb hakuna sare za Jeshi la Polisi,” alisema Lugola bungeni.

“Na mheshimiwa mwenyekiti nanyanyua mikono juu itakapofika jioni, kama mimi nasema uongo, najivua nguo.”

Advertisement

Kauli hiyo ilikuja kufuatia maelezo ya CAG, Profesa Mussa Assad alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Dodoma kusema kuna Sh16.66 bilioni zilizotakiwa kununua sare za jeshi hilo hazikuwa na ushahidi.

“Katika kaguzi maalumu kuna ununuzi wa sare za polisi uliofanywa na Jeshi la Polisi Tanzania. Hapa tulibaini kwamba lililipa Sh16.66 bila kuwepo kwa ushahidi wa uagizaji wa upokeaji wa sare hizo,” alisema Assad.

Hata hivyo, kauli ya Waziri Lugola ilikwenda kinyume na ile ya Rais John Magufuli aliyoitoa Julai 2016, alipokuwa akiwalisha kiapo cha uadilifu wa utumishi wa umma naibu makamishna wa polisi (DCP) na makamishna wasaidizi waandamizi (Sacp), ambapo alisema kuna mtu amelipwa fedha, lakini hakuna sare zilizonunuliwa.

Wachambuzi

Katika hilo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Abel Kinyondo alisema mawaziri wamekuwa wakizikosoa ripoti za CAG kwa sababu zinaangalia matumizi ya miaka ya nyuma, jambo ambalo alidai pia haliondoi makosa yaliyotajwa.

“Tatizo tulilonalo ni kwa sababu ni ripoti inayoangalia miaka ya nyuma, huwa ni rahisi sana kumpinga CAG kwa maana kwamba tuna miaka kama miwili mbele, kwa hiyo mtu anaweza kugundua kosa akalisahihisha, lakini kusahihisha kosa hakuliondoi,” alisema.

Alisema hata majibu ya maofisa masuhuli yanatakiwa yaakisi miaka ile ya uchunguzi wa kifedha na waeleze kwa nini huo mwaka wa fedha hakukununuliwa sare, hakukuwa na vithibitisho.

“Kwa mfano kama ripoti ikisema sare za polisi hazikutolewa hadi Juni 2018, halafu Julai au Agosti 2018 sare zikanunuliwa, hiyo haibatilishi lile kosa kwamba kulikuwa na ubadhirifu.”

Aliongeza kuwa ofisi ya CAG ni ya Serikali, hivyo mawaziri kujibu ripoti yake hadharani ni sawa na Serikali kujipinga yenyewe.

Aliwashauri mawaziri kufuata utaratibu wa kwenda kwenye kamati husika za Bunge watakakotoa malalamiko yao.

Mbali na Lugola, Spika wa Bunge, Job Ndugai alionyesha kutoridhishwa na hatua ya mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kutumia ripoti ya CAG kama rejea ya hoja zake kila wakati.

Hata hivyo, Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa ACT - Wazalendo alisema kauli hiyo ya Spika ni ya kukemewa.

“Nasikitika sana kauli za Spika na Lugola zinaweza kuwa hoja katika ripoti ya CAG. CAG anatoa hoja za ukaguzi. Anatoa nafasi ya Serikali kujibu hoja hizo. Kisha anatoa taarifa ya ripoti ya hoja ambazo hazikuwa na majibu. Mkaguzi anakuwaje mwongo? Hii ni lugha ya kukemea kabisa,” alisema Zitto.

“Nimekuwa mwenyekiti wa PAC/POAC kwa miaka minane mfululizo, muda mrefu zaidi kuliko Mtanzania mwingine yeyote. Asilimia100 ya hoja za CAG ni za kweli.”

Hivi karibuni, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka alisema si sahihi kwa mawaziri kujibu hoja za CAG na kwa kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu.

Katiba na sheria

Katiba kifungu cha 143 na vifungu vidogo(1 na 2) inataja kuwepo kwa CAG na majukumu yake kuwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya mfuko huo.

Kazi nyingine ni kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.

Pia, fedha ambazo matumizi yake yameidhinishwa na sheria iliyotungwa na Bunge na ambazo zimetumika, kwa ajili ya shughuli zilizohusika na matumizi ya fedha hizo na matumizi hayo yamefanywa kwa kufuata idhini iliyotolewa kuhusu matumizi hayo; na

Vilevile CAG anatakiwa angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Dodoma, Kaboyoka alisema kwenye Public Audit Act kifungu cha 38 (1) na (2) pia kwenye kanuni ya Katiba inawapa mamlaka PAC na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kuzungumzia juu ya taarifa za CAG na kuna utaratibu wake wa namna ya kujadili taarifa hizo.

Advertisement