VIDEO: Mwili wa meneja TFS waagwa, kuzikwa kesho Moro

Muktasari:

Mwili huo wa meneja wa TFS aliyefariki akizungumza na waandishi wa habari, umeagwa leo Dar es Salaam na mazishi yake yatafanyika kesho Mikese, Morogoro 

Mwili wa aliyekuwa meneja mawasiliano na uhusiano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Groly Mziray umeagwa leo jijini Dar es Salaam tayari kwa mazishi yatakayofanyika kesho Mikese, Morogoro.

Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kushiriki ibada hiyo ya kumuaga iliyofanyika katika kanisa la KKKT Mbezi Beach.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Mary Mwanjelwa alikuwa miongoni mwa waombolezaji akimuelezea marehemu kuwa alikuwa mtu mwenye jitihada na kupenda kujifunza.

“Nilisoma na Glory shahada ya pili, darasani alikuwa mwenye kujituma, kupenda kujifunza na kushirikiana na wenzake. Hivyo ndivyo vimemsogeza kufika mahali alipokuwa hadi kifo kimemkuta,”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Biashara TFS, Wilfred Emmanuel amemuelezea marehemu kama mfanyakazi aliyejitoa kwa dhati kwa ajili ya taasisi hiyo na alikuwa na mipango mingi ya kuipeleka mbali.

“Wiki iliyopita tulikuwa Morogoro kwenye bajeti alikuwa na mipango mingi na mizuri kwa ajili ya TFS, tutakachofanya ni kuitekeleza ili kumuenzi,” amesema Emmanuel.

Glory alizaliwa Desemba 27, 1980, ameacha mume na watoto wawili.