VITA YA KAGERA: Mashambulizi yaingia katika jiji la Entebbe -19

Muktasari:

Katika toleo lililopita tuliona Rais Julius Nyerere alivyolihutubia Taifa kuhusu tishio la Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi akimtaka aondoe majeshi yake Uganda ndani ya saa 24 la sivyo ataungane na Amin kuipiga Tanzania. Nyerere alimjibu kuwa Tanzania imeishi na Iddi Amin kwa miaka minane na kwamba inataka kumuonyesha kuwa vita si lelemama na akishajua hilo, madhali tuliishi naye miaka minane, tuko tayari kuishi naye miaka mingine minane.

SIKU nne baada ya Muammar Gaddafi kumwambia Rais Nyerere aondoe majeshi yake nchini Uganda ndani ya saa 24 la sivyo Libya itaingia vitani moja kwa moja kumsaidia Iddi Amin, ndege ya kijeshi ya Libya aina ya Tupolev Tu-22 ilipaa kutoka Uwanja wa Jeshi wa Nakasongola kwenda kupiga mabomu Tanzania.

Kwa mujibu wa kitabu cha War in Uganda: The Legacy of Iddi Amin, ndege hiyo ilikuwa ikiruka futi chache tu juu ya Ziwa Victoria kukwepa kuonekana kwenye rada. Nia yake ilikuwa ni kupiga mabomu matanki ya kuhifadhia mafuta yaliyopo Mwanza. Lakini rubani aliwahi kudondosha mabomu hayo ambayo yalianguka kwenye Kisiwa cha Saanane kilichopo ndani ya Ziwa Victoria.

Jarida la Summary of World Broadcasts: Non-Arab Africa liliripoti kwamba “Ndege ya Libya ya ‘Tupolev-22’ iliyotumwa (na Libya) kwenda Uganda kumsaidia Iddi Amin, jana saa 12:25 jioni ilirusha mabomu matano katika mji wa Mwanza eneo la Butimba katika Kisiwa cha Saanane.”

Jarida la Daily Report: People’s Republic of China liliandika kuwa, “Katika tukio hilo mtu mmoja alipata majeraha kichwani na mikononi ... vyanzo vya habari za kijeshi vinasema mabomu hayo yalikusudiwa kupigwa kwenye matanki ya hifadhi ya mafuta mjini Mwanza.”

Taarifa nyingine zilisema majeruhi pekee katika shambulio hilo alikuwa mfanyakazi wa hifadhi ya kisiwa hicho. Swala sita waliuawa pamoja na ndege kadhaa.

Tanzania ilijibu mapigo siku mbili baadaye. Ndege za Tanzania zilipaa kutoka Mwanza na kwenda kupiga mabomu katika miji ya Kampala, Jinja na Tororo. Kwa mujibu wa Xinhua Weekly, Aprili 2, 1979 ndege za Jeshi la Tanzania ziliupiga mabomu mji wa Jinja ambao ni wa pili kwa ukubwa na mji wa viwanda nchini Uganda, kiasi cha kilomita 70 Kaskazini mwa mji mkuu wa Kampala.

Katika mji wa Jinja, rubani wa Tanzania alifanikiwa kuipiga bomu Benki ya Maendeleo ya Libya-Uganda. Amin alikuwa mjini Jinja wakati mji huo ukishambuliwa. Hata hivyo, shambulizi hilo halikudumu kwa zaidi ya sekunde 10.

Kitendo cha ndege ya Tanzania kufanikiwa kulenga shabaha na kuitwanga Benki ya Maendeleo ya Uganda-Libya kiliwashangaza sana askari wa Amin kiasi cha kuwafanya waamini kuwa Tanzania ilikuwa na silaha kali.

Ndege zote za Tanzania zilirejea salama baada ya kufanya mashambulizi na siku mbili baadaye zikafanya shambulio jingine ndani ya Uganda. Safari hii uwanja wa ndege wa Entebbe ulishambuliwa, lengo likiwa ni kuuharibu ili ndege za Libya zisiweze kutua.

Kutoka kwenye miinuko ya Mpigi, Watanzania waliweza kuona mji wa Kampala kwa upande wa Kaskazini na Entebbe kwa upande wa Mashariki. Ndege za Libya zilionekana zikitua na kupaa na idadi kubwa ya askari wa Amin na wale wa Libya walikuwa Entebbe.

JWTZ iliona kuwa ikiwa wangeutwaa mji wa Kampala kabla ya ule wa Entebbe, askari wa Tanzania wangekabiliwa na jeshi kubwa la adui nyuma yao. Jenerali Msuguri aliamua waende kwanza Entebbe na kazi hiyo akakabidhiwa Brigedia Mwita Marwa wa Brigedi ya 208.

Kwa siku tatu mfululizo yalikuwa yakirushwa mabomu mawili au matatu kuelekea Entebbe. Wakati bomu moja lilipodondoka eneo la maegesho ya magari la Ikulu ya Entebbe, Amin akawa na uhakika kuwa wanajeshi wa Tanzania walikuwa wamemkaribia. Mara moja akatoka ndani ya Ikulu, akarukia kwenye helikopta iliyokuwa nje na kupaa kuelekea Kampala.

Jumanne ya Aprili 3, 1979 matangazo ya Redio Uganda yakasema, “Amin yuko mapumzikoni na ni mwenye furaha mjini Jinja.” Taarifa ikaendelea kusema, “Rais wa maisha wa Uganda amepuuza taarifa kwamba alikimbia na amewahakikishia wananchi wa Uganda kwamba yeye kama mshindi wa himaya ya Uingereza amejiandaa kufa akiitetea nchi yake.”

Ilipofika Aprili 6 mashambulizi ya Tanzania katika mji wa Entebbe yakaongezeka. Asubuhi iliyofuata Brigedi ya 208 ilikuwa inasonga mbele. Miongoni mwa mashambulizi waliyofanya siku hiyo ni kulipua gari la jeshi aina ya Land Rover lililokuwa na askari wanane wa Libya wakielekea Mpigi.

Siku hiyo ndege ya mizigo ya Libya, C-130, ikatua uwanja wa Entebbe saa nne asubuhi kujaribu kuwaokoa askari wa Libya walionasa. Askari 30 wa Libya walikazana kuingia ndani ya ndege hiyo kabla haijageuka na kuanza kuondoka. Lakini askari wa Tanzania walikuwa wameshalikaribia eneo hilo na kuilipua. Ndege hiyo ilishika moto ikawateketeza askari wote wa Libya waliokuwa ndani yake.

Mashambulizi kutoka kwa askari wa Tanzania yalipoongezeka, askari wa Libya waliobaki Entebbe walizidi kuchanganyikiwa. Waliingiwa na wazo la kukimbilia Kampala lakini hawakujua njia watakayoifuata kufika huko.

Entebbe ilipozingirwa vya kutosha, askari wa Libya waliobaki nao waliamua kutafuta njia ya kukimbilia Kampala. Malori kadhaa yaliyowabeba askari wa Libya yakisindikizwa na magari mawili ya deraya yalianza safari kuelekea Kampala.

Umbali wa kilomita nane kutoka Entebbe, Luteni Kanali Salim Hassan Boma aliwasubiri. Aliwagawa wapiganaji wake wakae pande mbili za barabara.

Msafara uliowabeba askari wa Libya ulipofika eneo walikojificha askari wa JWTZ, askari wa Tanzania walikaa kimya na bila kujigusa. Makamanda wa Libya walisemezana kwa muda mfupi, kisha askari waliokuwa kwenye magari hayo wakaanza kumimina risasi pande zote mbili za barabara.

Hazikuwagusa askari wa Tanzania. Lakini wakiwa na wasiwasi bado waliruhusu gari moja likatangulia. Walipoona hakuna kinachoendelea, makamanda wa askari wa Libya wakaruhusu magari mengine yaliyojaa askari wao yapite.

Ndipo Luteni Kanali Salim Hassan Boma akatoa amri ya kufanya shambulio. Magari yote ya kivita ya Libya yakashambuliwa na kuteketea kwa moto hata kabla hawajaweza kujibu shambulizi lolote.

Harufu ya kuungua kwa nyama ikatawala eneo hilo. Ndani ya dakika 10 askari wote 65 wa Libya wakawa wamekufa.

Itaendelea kesho