Wabunge washangazwa kutolea Sh100milioni za maendeleo badala ya Sh19.6bilioni bajeti Wizara ya Madini

Muktasari:

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imesema utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo ya Wizara ya Madini hauridhishi kutokana na wizara hiyo kupokea chini ya asilimia moja ya fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya 2018/2019

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imesema utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo ya Wizara ya Madini hauridhishi kutokana na wizara hiyo kupokea chini ya asilimia moja ya fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya 2018/2019.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 27, 2019 na makamu mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Mariam Ditopile  bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha  maoni ya kamati hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2019/2020.

Amesema kiasi cha fedha za miradi ya maendeleo kilichopokelewa katika kipindi cha kati ya Julai 2018 hadi Februari, 2019 ni Sh100milioni sawa na asilimia 0.5 ya bajeti yote ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2018/2019 ambayo ni Sh 19.6bilioni.

Amesema hali hiyo imesababisha ucheleweshwaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na miradi mingine kutotekelezwa kabisa.

“Kamati inafahamu Sh8.6bilioni kilitengwa kwa ajili ya uchenguaji wa visusu vya dhahabu katika mgodi wa Buhemba na kiasi hicho kinakusudiwa kutumika kama mtaji wa Stamico wakati  mazungumzo na majadiliano ya ubia kati ya mwekezaji na Stamico yatakapokamilika,” amesema.

Amesema kamati hiyo inaona kuwa mazungumzo hayo yamechukua muda mrefu jambo ambalo linaweza kuleta athari katika uwekezaji huo.

Amesema wanaishauri Serikali izingatie utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo kama zinavyoidhinishwa na Bunge ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati kama ilivyokusudiwa.