Profesa Mukandala: Hatua sahihi ununuzi Mv Bukoba hazikufuatwa

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jakaya Kikwete (kushoto) akizungumza jambo na mtangulizi wake katika chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala baada ya kumalizika kwa muhadhara wa uprofesa leo Mei 21, 2024 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Meli ya Mv Bukoba ilizama Mei 21, 1996 ikiwa karibu kuingia ghuba ya Mwanza na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800. Wengi wao wamezikwa katika makaburi yaliyopo Igoma, Mwanza.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala amesema hatua za kawaida na sahihi za ununuzi wa meli ya Mv Bukoba hazikufuatwa na Serikali.

Amesema licha ya mkataba huo kutokuwa na usawa, masharti yake yalikuwa magumu kwa mnunuzi.

Profesa Mukandala amesema hayo leo Jumanne, Mei 21,2024  wakati akiendesha muhadhara wa uprofesa uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Nkrumah uliopo ndani ya UDSM.

Mhadhara huo ni juu ya dola, soko, kushindwa kwa taasisi, mafunzo kutoka katika kujifungua kwa uchungu wa kushinikiza, maisha ya mateso, na kifo cha maumivu cha Mv Bukoba, umewasilishwa mbele ya wasomi, viongozi wa kitaifa na vyuo mbalimbali.

Profesa Mukandala amesema kutofuata matakwa ya msingi ya kutonunua bidhaa sokoni, machapisho kuhusu manunuzi ya umma yanaonyesha hakukuwa na ununuzi wa bidhaa katika ushindani wa zabuni.

“Serikali haikufuata mchakato wa manunuzi uliozoeleka, mkopo ulikuwa na masharti magumu, meli na nanga zake zilipaswa kununuliwa kutoka Ubelgiji, isitoshe hata huko hakukuwa na ushindani wowote, Serikali ya huko iliteua kampuni ya kutengeneza meli hiyo, “ amesema.

“Mnunuzi ambaye ni Serikali ya Tanzania haikuwa na kauli yoyote kuhusu hilo kwenye mpangilio huo, kampuni iliyojulikana MS Belgium Shipping builders Cooperation iliyokuwa muunganiko wa watengenezaji meli watatu, iliteuliwa na Ubelgiji ijenge meli hizo tatu, hata hivyo haifahamiki ni kwa namna gani kampuni hiyo ilifahamika na Serikali hiyo na ni kwa namna gani iliteuliwa,” amesema Profesa Mukandala.

Amesema Shirika la Reli Tanzania, liliingia kwenye mazungumzo na mawakala wa BS wanaotengeneza meli, Shirika la Reli liliainisha vigezo vilivyotakiwa pamoja na namna itakavyobeba mizigo na abiria pamoja na idadi ya mabehewa na mgawanyiko wake.

Amesema kampuni hiyo ilichora mchoro meli hiyo itakavyokuwa, japo hakuna uhakika kama ilipitiwa na vigezo vile vinavyotakiwa, kwa kuwa masuala ya kiufundi yanatakiwa kujadiliwa kwa kina.

Profesa Mukandala amesema hatua ya pili ilikuwa kutengeneza mkataba, akisema ni eneo muhimu linalohitaji kuchunguzwa na kwamba, mazungumzo yalifanyika kati ya Shirika la Reli.

“Machi mwaka 1976 kampuni hiyo ilituma mkataba chini ya mazingira ya dharura, wakitaka uwe umesainiwa ifikapo tarehe 21 mwezi huohuo haikutaka mabadiliko yoyote kwenye masharti ya mkataba huo,” amesema.

Amesema pale ulipokuwa haujasainiwa hadi tarehe ya mwisho wa mkataba, kampuni hiyo ilishinikiza ifikapo Mei 15 mwaka huohuo mkataba uwe umesainiwa.

Profesa Mukandala amesema suala hilo liliwafanya wawakilishi wa wateja upande wa Tanzania, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Shirika la Reli Tanzania kukaa kwa pamoja na kufanya tathmini.

“Mkataba huo ulikuwa hauna usawa, Waziri wa Uchukuzi alielekeza mkataba usainiwe, hilo lilikuwa pia agizo kutoka kwa Mkuu wa nchi kwamba mkataba usainiwe mara moja, hii inapaswa tuangalie kwa nchi yetu kwa maana Rais alipewa mamlaka hayo kikatiba,” amesema Mukandala.