Wachezaji Taifa Stars kulamba milioni 10 kila mmoja iwapo watafuzu

Muktasari:

Kesho Jumapili, Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itacheza na timu ya Uganda ‘The Cranes’ kuwania kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika nchini Misri mwezi Juni, 2019`

Dar es Salaam. Wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea kambi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde, Paul Makonda amesema watatoa kiasi cha Sh10 milioni kwa kila mchezaji iwapo wataichapa Uganda ‘Cranes’ kesho Jumapili na kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Misri.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Machi 23, 2019 na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema Majaliwa amewaeleza wachezaji na benchi la ufundi kuwa Serikali ina imani nao na wasiwe na wasiwasi kwa sababu hawana tofauti yoyote na wachezaji wa timu nyingine duniani.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa maendeleo makubwa yanayoendelea kupatikana katika soka nchini.

“Macho yote ya Watanzania yameelekezwa katika mechi ya kesho na Serikali ina matumaini makubwa na timu ya Taifa, hivyo waelewe kwamba kesho ni siku muhimu sana. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo mataifa mengine yamefikia,” amesema Majaliwa.

Kwa upande wake, Makonda ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema kamati yake itatoa sh. milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo iwapo timu itafuzu kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON)

Makonda amesema Watanzania wanachokijua kwa sasa ni kwamba AFCON 2019 ni zamu yao, hivyo amewaomba wachezaji wa Taifa Stars wahakikishe wanawapa furaha kwa kuifunga timu ya Taifa ya Uganda na kwamba wananchi wengi wamehamasika kwenda kuwashangilia.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangala ameahidi kuwapeleka katika mbuga ya wanyama kwa ajili ya mapumziko iwapo wachezaji hao wataibuka na ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda hapo kesho.

Dk Kigwangala amesema Serikali ipo pamoja na wanamichezo, ambapo amewataka wachezaji hao wa timu ya Taifa wakapigane kweli kweli kwa ajili ya Taifa lao. “Kesho muingie uwanjani kama askari wa nchi. Mkapiganie ushindi wa Taifa letu”.

Awali, Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samata amesema, “Nina furaha si kwa sababu ya ukubwa wa mechi ya kesho bali ni kwa sababu naona kesho nakwenda kuongoza nchi. Tupo tayari kuliletea Taifa ushindi”.