Wafanyabiashara wa Kariakoo wamlilia Majaliwa

Muktasari:

  • Katika mkutano huo, Makonda alipendekeza taratibu za upatikanaji leseni za wafanyabiashara katika mkoa huo ufanyike ndani ya saa 24, tofauti na usumbufu wanaokutana nao waomba leseni hizo kwa sasa.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa kati na wadogo wa Kariakoo jijini Dar es Salaam jana walitoa ‘ya moyoni’ kuhusu mazingira magumu wanayokutana nayo ikiwamo vikwazo vya malimbikizo ya kodi, uanzishaji wa biashara, vishawishi vya utoaji wa rushwa na urasimu katika mamlaka zinazohusika katika sekta ya biashara nchini.

Aidha wamependekeza kuangaliwa upya viwango vya kodi vinavyoongezwa kwa wafanyabiashara ilhali mapato yamekuwa hayatabiriki katika mazingira ya kibiashara nchini. Wafanyabiashara hao walibainisha dosari hizo katika mkutano maalumu ulioandaliwa kati ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na wafanyabiashara wa manispaa hiyo kwa lengo la kupokea changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.

Mwenyeji wa mkutano huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliyekuwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya hiyo ya Ilala, Sophia Mjema.

Mfanyabiashara, Khatibu Omary aliomba wafanyabiashara wajulishwe mapema taarifa za malimbikizo ya kodi wanazodaiwa badala ya kusubiri miaka mitano hali inayoshawishi mazingira ya kutoa rushwa.

Katika mkutano huo, Makonda alipendekeza taratibu za upatikanaji leseni za wafanyabiashara katika mkoa huo ufanyike ndani ya saa 24, tofauti na usumbufu wanaokutana nao waomba leseni hizo kwa sasa.

“Tulishaleta maombi kwa wizara ya viwanda, ufupishwe muda kidogo, tupate ndani ya saa 24 au ikizidi sana ndani ya saa 48, ukianza process za leseni ni ngumu na ndiyo maana watu wanatamani wakwepe tu kodi kwa sababu utaratibu wa kupata tu leseni ni mgogoro utafikiri unataka kutoa rushwa ili upate leseni,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa aliyeagiza kusimamishwa kazi mmoja kati ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa tuhuma za rushwa, alisema Serikali haitakuwa tayari kuona vikwazo vikiendelea kwa wafanyabiashara nchini.

Pia aliwaahidi kuyawasilisha maoni yao mbele ya vikao vya Bunge lijalo kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi na Serikali.

“Mkakati wowote wa serikali katika kukuza uchumi unawategemea wafanyabiashara na mipango ya serikali ni kuufanya mkoa huo kama hub (kituo) ya kibiashara nchini hivyo hatua inayofanyika kwa sasa ni kuhakikisha vikwazo vyote vinashughulikiwa,” alisema Majaliwa.