Wafanyakazi waiomba TAA ishikilie ndege za Fastjet
Muktasari:
Wafanyakazi wa Fastjet PLC wameiomba Mamlaka ya Anga kuendelea kuzishikilia ndege mbili mali ya Fastjet PLC ambazo moja ipo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere na nyingine Nairobi hadi hapo kampuni hiyo itakapolipa madeni yote inayodaiwa ikiwamo haki zao wafanyakazi.
Dar es Salaam. Wafanyakazi wa kitanzania wa kampuni ya Fastjet wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Kazi kuwasaidia wapate haki zao.
Pia, wameiomba Mamlaka ya Anga kuendelea kuzishikilia ndege mbili mali ya Fastjet PLC ambazo moja ipo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere na nyingine Nairobi hadi hapo kampuni hiyo itakapolipa madeni yote inayodaiwa pamoja na haki zao wafanyakazi.
Hayo yalisemwa leo Machi Mosi na Mohamed Ngamanya ambaye ni ‘senior cabin crew’ wa shirika hilo kwa niaba ya wenzake.
Nganyama alipinga kauli ya Lawrance Masha kuwa wamelipwa mishahara ya Januari na Februari, mwaka huu.
“Ukweli ambao tunao sisi wafanyakazi, Januari alilipa asilimia 50 kwa baadhi ya wafanyakazi na Februari hakuna aliyepata mshahara,” alisema Nganyama.
Aĺisema wafanyakazi wa Fastjet PLC ambayo makao makuu yake yapo Afrika Kusini, wanamtambua Masha kama mfanyakazi mwenzao kwa sababu naye analipwa mshahara kama wao.
Hivyo wao wanaitambua Fastjet PLC kama inavyotambuliwa na mamlaka zinazoshughulika na anga kuwa ndiyo mmiliki wa kampuni hiyo na si Masha.
Ofisa Mwendeshaji shughuli za anga wa kampuni hiyo, Tiba Hobo aliiomba
Serikali iweze kuingili kati iwapate Fastjet PLC kusudi waweze kumalizana na wafanyakazi wake.
Kwa upande wa Ofisa Rasirimali watu wa shirika hilo, Emmanuel Muhindi yeye alikiri kuwa wafanyakazi hao Januari mwaka huu baadhi hawajalipwa mishahara na wengine wamelipwa asilimia 50 na kwamba, waliahidi kuwalipa lakini hawakufanikiwa.
Muhindi amesema Februari, mwaka huu, hakuna mfanyakazi aliyelipwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha na jana waliwaeleza kwa njia ya email kuwa siku chache zijazo watataarifiwa nini kitakachofuata.