Wafugaji Manyara waandamana kumpongeza Rais Magufuli

Wafugaji wa Kijiji cha Kimotorok Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakionyesha mabango wakati wakiandamana kumpongeza Rais John Magufuli.Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Wafugaji wa wilaya za Simanjiro, Mbulu, Kiteto na Hanang' mkoani Manyara, leo wamefanya maandamano katika maeneo yao kumpongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wake wa kutowafukuza kwenye maeneo ya hifadhi

Manyara. Wafugaji wa wilaya za Simanjiro, Mbulu, Kiteto na Hanang' mkoani Manyara wameandamana leo kwa ajili ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuzuia wafugaji wanaoishi pembezoni au ndani ya hifadhi wasihamishwe wala kufukuzwa.

Maandamano hayo ambayo yamefanyika katika maeneo tofauti ya wilaya hizo na kwenda ofisi za vijiji, Serikali za mitaa au viwanja vya wazi wakiwa na mabango.

Diwani wa kata ya Endamilay wilayani Mbulu, Gesso Bajuta ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu amesema Rais Magufuli asifanye kampeni kwenye uchaguzi wa urais mwaka 2020 kwani amedhihirisha ni mtetezi wa wanyonge.

"Wanyonge watampitisha Rais Magufuli bila kupingwa Tanzania nzima kwani amedhihirisha kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge kwa vitendo, awali wafugaji walinyanyasika kwa muda mrefu," amesema Bajuta.

Amesema kwa muda mrefu wafugaji nchini wamepata tabu na changamoto nyingi zinazotokana na kuondolewa kwa nguvu wakati mwingine kuharibiwa mali zao kwa kisingizio siyo maeneo ya mifugo.

Mwenyekiti wa chama cha wafugaji nchini, George Bajuta ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hanang' amesema Rais Magufuli amewakuna wafugaji na kuonyesha ni mtetezi wa wanyonge.

Bajuta amesema wafugaji wameandamana kwa amani ili kumpongeza Rais Magufuli kama ishara ya kuonyesha kufurahishwa kwao na tamko lake.

Amesema wafugaji kwa kushirikiana na chama chao na mashirika ya kutetea wafugaji wameungana kumpongeza Rais Magufuli kwani Serikali ya awamu ya tano imetambua changamoto wanazopata wafugaji nchini.

Diwani wa Loiborsiret  wilayani Simanjiro, Ezekiel Lesenga Mardad amempongeza Rais Magufuli kwani wananchi wa kata yake walikuwa wanateseka kupitia mgogoro wa mpaka na hifadhi ya jamii ya Mkungunero iliyopo wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma.

"Wananchi wangu hasa wa kijiji cha Kimotorok walikuwa kwenye wakati mgumu lakini kupitia kauli ya Rais Magufuli hivi sasa wamezaliwa upya kwa kauli yake ametukosha mno," amesema Mardad.

Diwani wa Terrat wilayani Simanjiro, Jackson Ole Materi amesema katika maisha yake hajawahi kufurahi kama siku Rais Magufuli alipotoa tamko hilo la kuwalinda wafugaji nchini.

Ole Materi amesema zaidi ya vijiji 389 vya wafugaji vina migogoro na hifadhi za Taifa na hifadhi za jamii ila kwa kauli ya Rais Magufuli migogoro hiyo itamalizika kupitia uhakiki mpya utakaofanyika.