Wafungwa, mahabusu 340 wakutwa na Ukimwi

Muktasari:

  • Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi leo Jumanne imetembelea Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira mkoani Morogoro na kuelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kuwa kati ya wafungwa na mahabusu 15,250 waliopimwa, 340 wamekutwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU)

Dar es Salaam. Wafungwa na mahabusu 340 kati ya 15,250 nchini waliopimwa Virusi vya Ukimwi (VVU) wamekutwa na maambukizi baada ya Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Wizara ya  Afya, kutoa elimu ya upimaji katika Magereza mbalimbali nchini.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ameyasema hayo leo Jumanne  Machi 4, 2019 wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya maambukizi ya VVU na upatikanaji wa tiba ya magonjwa nyemelezi na udhibiti wa biashara na matumizi ya dawa za kulevya magerezani kwa mwaka ulioisha.

Masauni ameieleza Kamati  ya Kudumu  ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi iliyofika katika Gereza Kuu la Wanawake Kingolwira mkoani Morogoro kuwa kati ya mahabusu na wafungwa waliopima, wanaume waliokutwa na maambukizi ni 292 na wanawake ni 48

“Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Afya wanahakikisha huduma za afya zinaboreka magerezani ikiwemo lishe nzuri kwa wanaothibitika wana maambukizi pamoja na matumizi ya dawa za kufubaza makali ya Ukimwi,’’ amesema Masauni.

 “Elimu ya kifua kikuu na upimaji inatolewa kila siku magerezani kwa wafungwa na mahabusu, kwa mwaka jana jumla ya waliopima ni 12,870 huku waliobainika na maambukizi ni 167.”

“Tunashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) kwa kuandaa Mpango Mkakati wa Ukimwi na kifua kikuu kwa miaka mitano,” amesema Masauni.

Wakizungumza kwa nyakati tofuati wajumbe wa  kamati hiyo wamelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuwahudumia mahabusu na wafungwa wanaoishi na maambukizi magerezani huku wakitoa wito kwa wafungwa walioathirika kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao kuhusiana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Afya na Lishe wa Jeshi la Magereza, Dk Hassan Mkwiche amesema magereza yana utaratibu wa kupima afya za mahabusu au wafungwa siku ya kwanza tu anayoingia gerezani  ikiwemo ujauzito, Ukimwi, kifua kikuu na magonjwa mengine ili waweze kuhudumia kila mfungwa na mahitaji yake.

“Mfungwa anapoingia humu anaenda kukutana na kazi mbalimbali kwa hiyo ni muhimu kujua afya ya kila mmoja tangu siku ya kwanza anaingia ili kuweza kumpangia majukumu kulingana na afya yake lakini pia aina ya mlo anaotakiwa ale akiwa kifungoni,” amesema Dk Mkwiche.