Waislamu Manyara waomba mvua ya neema

Sunday March 24 2019

 

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Babati. Imeelezwa kuwa ukame uliopo nchini unaletwa na vitendo viovu vinavyofanywa na binadamu hivyo kusababisha mvua kutonyesha.

Sheikh wa mkoa wa Manyara, Mohamed Kadidi ameyasema hayo leo Machi 24 kwenye ibada ya kuomba mvua ya neema iliyofanyika Uwanja wa Kwaraa mjini Babati.

Sheikh Kadidi amesema vitendo viovu vya binadamu ikiwemo uharibifu wa mazingira husababisha kukosekana kwa mvua na kuwepo kwa ukame.

"Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie mvua ya neema isiyo na madhara nchini Tanzania ambayo itasaidia wakulima wapate mazao waliyopanda kwenye wakati huu wa masika," amesema Sheikh Kadidi.

Amesema mvua zimegoma kunyesha sehemu nyingi kutokana na vitendo viovu vinavyofanywa na binadamu ikiwemo ukataji ovyo wa miti na kutotunza mazingira yanayozunguka jamii.

"Tunapaswa tumrudie mola wetu kwa kufanya ibada na kuachana na matendo maovu ili tuishi kwa raha mustarehe kama zamani ambapo kulikuwa na misimu miwili ya masika kwa mvua kunyesha za kutosha," amesema Sheikh Kadidi.

Advertisement

Baadhi ya waumini walioshiriki maombi hayo wamesema jamii inapaswa kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa wingi na kuepuka ukataji ovyo wa miti.

Mkazi wa mtaa wa Miyomboni, Abdalah Hussein amesema watu wengi wanaharibu mazingira ikiwemo ya Mlima Kwaraa ambao ni chanzo cha maji yanayohudumia mji wa Babati na pembezoni.

"Watu wengi wanapenda vivuli vya miti lakini hawapendi kupanda miti, tunapaswa kubadilika juu ya hilo kwa kupanda miti kwa wingi," amesema Hussein.

Mkazi wa Magugu Ally Hassan amesema jamii inapaswa kulazimishwa kupanda miti na kuitunza ili kufanikisha mazingira bora na mvua kunyesha ili kuepukana na ukame.

"Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Vrajlal Jituson amewahi kuendesha kampeni ya kugawa bure miche ya matunda na kuagiza kuwa jamii italipia endapo miti hiyo itakufa hivyo kusababisha watu wengi kuhofia na kutunza miche hiyo," amesema Hussein.

Advertisement