Walichokisema Chadema wakurugenzi kupigwa ‘stop’ kusimamia uchaguzi

Muktasari:

  • Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeipongeza Mahakama Kuu ya Tanzania kufuta sheria iliyowapa wakurugenzi wa halmashauri mamlaka ya kuwa wasimamizi wa uchaguzi

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeipongeza Mahakama Kuu ya Tanzania kufuta sheria iliyowapa wakurugenzi wa halmashauri mamlaka ya kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Mei 12, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano, uenezi na mambo ya nje wa chama hicho, John Mrema amesema: “Tunaipongeza Mahakama Kuu kwa namna ilivyosimamia Katiba wakati tunajiandaa kupigania tume huru ya uchaguzi, kama chama yapo ambayo yanapaswa kutazamwa.”

Amesema sheria ya uchaguzi  inazuia watu wote wanaojihusisha na uchaguzi kujihusisha na chama cha siasa.

Amesema wanao ushahidi wakurugenzi  86 ambao ni wanachama wa chama kimoja cha siasa nchini waligombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 na kukosa na wakateuliwa kuwa wakurugenzi.

"Kama Mahakama isingebatilisha makada hawa wangekuwa ndio wasimamizi katika uchaguzi ujao," amesema Mrema.

Jaji Atuganile Ngala ambaye alisaidiana na majaji Benhajj Masoud na Firmin Matogolo alitoa uamuzi huo Ijumaa Mei 10 katika kesi hiyo ya kikatiba iliyofunguliwa mwaka jana.

Katika kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mwanachama wa Chadema, Bob Wangwe aliyekuwa mdai pekee, alikuwa anapinga wakurugenzi hao wa halmashauri za wilaya, manispaa na au majiji kuwa wasimamizi akidai kuwa ni kinyume cha Katiba.

Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za Wangwe dhidi ya utetezi wa Serikali iliyojitetea kuwa suala hilo haliathiri uchaguzi kwa kuwa uteuzi wao ni kwa mujibu wa sheria.

Jaji Ngwala alisema vifungu 7(1, kinachowapa wakurugenzi mamlaka ya kusimamia uchaguzi na 7(3) vya Sheria ya Uchaguzi vinakwenda kinyume na matakwa ya kikatiba ya uhuru wa Tume ya Uchaguzi.

Alisema wakurugenzi hao ni wateule wa Rais na hawako chini ya Tume, wakati Katiba inaelekeza NEC iwe chombo huru.

Jaji Ngwala pia alisema sheria hiyo haihakikishi kuwa wakurugenzi hao wanakuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema wameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mdai kuwa wakurugenzi wengi ni wanachama wa CCM baada ya mahakama kupewa orodha ya wakurugenzi 74 wanachama wa chama hicho tawala.

Kifungu 7(3) kinaeleza kwamba NEC inaweza kumteua mtu yeyote kuwa msimamizi, lakini Mahakama ilisema hakiweki ulinzi kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa huru na kwamba lazima kuwe na ulinzi kwa kuhakikisha kuwa anayeteuliwa si mwanachama wa chama chochote cha siasa.