Walichokisema mahakamani wadhamini wa Lissu hiki hapa

Muktasari:

  • Wadhamini wa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lisu leo Jumatatu wamefika mahakamani kuieleza Mahakama hali ya Lissu inaendeleaje.

Dar es Salaam. Wadhamini wa Tundu Lissu wamefika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuieleza Mahakama sababu za Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) kutofika mahakamani.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Saimon amedai leo Jumatatu, Februari 25, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba kuwa kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na tarehe iliyopita Mahakama ilitoa amri ya wadhamini wa Lissu kufika mahakamani kueleza hali yake.

Februari 4, 2019 Hakimu Simba aliamuru wadhamini wa Lissu kufika mahakamani hapo kueleza hali ya mbunge huyo kwa kuwa Mahakama hiyo haina rekodi ya taarifa.

Leo wadhamini hao waliitikia wito na kufika mahakamani hapo ambapo mdhamini wa kwanza Ibrahimu Ahmed na Robert Katula wameeleza kuwa Lissu yuko kwenye matibabu nchini Ubelgiji.

Pia wadhamini hao wameomba radhi baada ya Hakimu kutaka kujua sababu za wao kutofika Mahakamani hapo kwa zaidi ya miezi minane bila taarifa yoyote.

Akijitetea Ibrahimu amesema anauguliwa na mzazi wake na hadi sasa amelazwa wakati mdhamini wa pili Katula yeye akiomba radhi mahakama kwa kutojua.

Hakimu Simba aliwaonya wadhamini na kuwataka kufika mahakamani kila kesi itakapotajwa na kuiahirisha hadi Machi 25, 2019.

Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

 

Inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi.

Lissu yupo nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Siku hiyo hiyo Lissu alipelekwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu akitokea Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.

Lissu ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chadema alikaa Kenya hadi Januari 6 mwaka 2018 alipohamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambako yupo mpaka sasa.