Lugola ashangaa Tundu Lissu kutokamatwa mpaka sasa

Muktasari:

Wakati mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akiendelea na ziara zake nchini Marekani, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Kangi Lugola amemtaka kurejea nchini ili kusaidia upelelezi wa tukio lake la kushambulikwa kwa risasi

Arusha. Siku 524 tangu Tundu Lissu apigwe risasi jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amelishangaa Jeshi la Polisi kushindwa kumkamata mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema).

Lugola alitoa kauli hiyo jana jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara yake mkoani hapa na tukio la mwanasheria mkuu huyo wa Chadema kupigwa risasi.

Lugola pia alitumia mkutano huo kujibu hoja za Lissu alizozitoa Marekani anakofanya ziara kuzungumzia tukio la kushambuliwa kwake pamoja na masuala ya siasa na utawala bora nchini.

“Kama amepata nafuu (Lissu) badala ya kuanza uzembe za uzururaji alipaswa kuja (nchini). Nashangaa polisi kila siku wanahangaika kukamata vijana kwa uzururaji na kumuacha huyu (Lissu),” alisema Lugola.

Lissu alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, jijini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge akiwa na dereva wake Adam Bakari ambaye hakujeruhiwa.

Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyohiyo usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, mwaka jana alipohamishiwa Ubelgiji.

Desemba 31, mwaka jana aliruhusiwa kutoka hospitali huku akieleza kuwa amepewa ruhusa licha ya kuwa bado yupo katika matibabu na akaanza ziara Ulaya na Marekani.

“Dereva huyu atueleze kwa nini alipoona gari linawafuata kwa nyuma (alipokuwa na Lissu wakitokea bungeni) hakukimbilia kituo cha polisi kilichopo jirani na nyumba aliyokuwa akiishi Lissu,” alisema Lugola.

Alisema dereva huyo anapaswa kueleza sababu za Lissu kupigwa risasi nyingi, huku yeye akitoka mzima bila jeraha lolote la risasi na walikuwa gari moja.

“Kwa hali ya kawaida tu ni jambo la kushangaza, risasi zote hizo wanasema 38 hakuna hata iliyomgusa (dereva),” alisema Lugola.

Lugola alisema iweje Lissu ashambuliwe upande wa kulia na risasi kumpiga zaidi mguu mmoja wa kushoto tu badala ya mguu wa kulia.

Alisema katika gari alilokuwemo mbunge huyo kuna kisanduku kinachotenganisha anapoketi dereva na abiria wa mbele, akahoji sababu za kisanduku hicho kutoguswa na risasi.

Lugola pia alipinga taarifa kuwa katika eneo alilokuwa akiishi Lissu kuna kamera za CCTV.

“Nyumba zote za wakala wa majengo mkoani Dodoma hazina CCTV. Huu ni upotoshwaji mkubwa ambao unalenga kuwadanganya wananchi na kuwataka waichukie Serikali yao na Rais John Magufuli, mimi kama Waziri wa Mambo ya Ndani sitakubali,” alisema.

Alisema hoja ya Lissu na dereva wake kuwa eneo hilo lilikuwa linalindwa na polisi na siku ya tukio hawakuwepo ni ya uongo, akibainisha kuwa waliokuwa wakilinda ni walinzi binafsi.

“Kutokana na utata ndio maana tumekuwa tukiwataka Lissu na dereva wake kutoa maelezo ili kukamilisha upelelezi. Wao ndio wahusika badala ya kutoa maelezo nchini wanatoa maelezo nje ya nchi,” alisema.

Lugola alisema katika mikutano ya Lissu nchini Marekani anawapanga watu wanaomuunga mkono ili aonekane ni mtu anayekubalika na watu wengi.

Kuhusu sababu za kumjibu Lissu, Lugola alisema amefanya hivyo kwa kuwa mbunge huyo na dereva wake wanazungumza mambo ya uongo. “Lazima (Lissu) aje kwenye kesi yake na yeye ndiye shahidi muhimu.

Anasema eti angekufa tusingechunguza, kwanza lazima atambue hakufa na ni lazima uchunguzi wa tukio lake ungefanyika tu kama ilivyo matukio mengine,” Lugola.

Lugola pia alizungumzia jinsi alivyolitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwakamata watu wanaotoa kauli za uchochezi.

Kuhusu matukio ya uhalifu alisema mwaka 2017 yalikuwa 596,533, mwaka 2018 matukio 591,803 ikiwa pungufu kwa matukio 4730.

Alisema matukio madogo ya uhalifu yalikuwa 529,393 mwaka 2017 na 531,935 mwaka jana.