Wananchi wamsusia mkutano DC Same

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule amejikuta  katika wakati mgumu baada ya wananchi waliohudhuria mkutano wake kumkimbia kwa madai kuwa aliwapa majibu yasiyoridhisha kuhusu matukio ya ushirikina

Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule amejikuta  katika wakati mgumu baada ya wananchi waliohudhuria mkutano wake kumkimbia kwa madai kuwa aliwapa majibu yasiyoridhisha.

Tukio hilo lililothibitishwa na Rosemary limetokea jana Jumanne Juni 2, 2019 kata ya Mpinji wilayani Same  alikokwenda kutatua mgogoro uliotokana na imani za kishirikina baada ya kutakiwa kufika eneo hilo na wananchi.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano Julai 3, 2019 baadhi ya wananchi hao wamesema walitarajia kupata msaada wa Serikali kutokana na kuchoshwa na vitendo vya ushirikina vinavyofanywa na baadhi ya wenzao.

Amina Mgonja, amedai walipanga kuwafukuza wachawi waliopo katika eneo hilo kwa kutumia waganga wa jadi.

“Ili kufanikisha zoezi hili tuliomba kibali cha  mkuu wa wilaya, alikuja mkutanoni kuzungumza na sisi lakini tulipowasilisha malalamiko yetu alitueleza kuwa Serikali haiamini uchawi.”

“Alitueleza kama tumekereka na sisi tukanunue uchawi. Kwa kweli kauli hiyo ilisababisha wananchi wote tuliokuwa katika mkutano kuondoka,” amesema Amina aliyezungumza kwa niaba ya wenzake.

Katika maelezo yake mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali haiamini uchawi, “Ni kweli hali hiyo ilijitokeza  lakini mimi nilikua natimiza wajibu wangu kisheria kama Serikali tunalikemea jambo hilo kwa nguvu zote.”