Wanawake wawili kizimbani Kisuti kwa kosa la utakatishaji fedha

Muktasari:

  • Wanawake wawili wakazi wa Tegeta, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba, likiwemo la kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha kiasi cha Sh25milioni.

Dar es Salaam. Wanawake wawili wakazi wa Tegeta, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba, likiwemo la kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha kiasi cha Sh25milioni.

Washtakiwa hao ni Veronica Tembe (45) na Lilian Kisamo (41), wote ni wafanyabiashara na wakazi wa Tegeta.

Akiwasomea hati ya Mashtaka jana Jumatatu Juni24, 2019,  wakili wa Serikali, Faraji Nguka akisaidiana na Saada Mohamed, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile kuwa katika shtaka la pili, inadaiwa siku na mahali pasipojulikana mshtakiwa Veronika peke yake akiwa na nia ovu, alighushi kadi ya gari aina ya Toyota Rav4 kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa kadi hiyo ni halisi na imetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Pia, Veronika anadaiwa Novemba 27,2012  Katika Benki ya EFC microfinance iliyopo eneo la Victoria ndani ya Wilaya ya Kinondoni,  aliwasilisha kadi hiyo ya kughushi ya gari kwa maofisa wa EFC.

Katika shtaka la nne, mshtakiwa Veronica alighushi leseni ya biashara kwa lengo la kuonyesha kuwa leseni hiyo imetolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, wakati akijua ni uongo.

Pia, Veronica anadaiwa Novemba 27, 2012 katika ofisi ya EFC Tanzania Microfinance Ltd iliyoko eneo la Victoria mshtakiwa aliwasilisha leseni ya biashara ya kughushi kwa ofisa wa benki ya EFC kwa madhumuni ya kuonesha kuwa leseni hiyo imetolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala huku akijua kuwa siyo kweli.

Katika shtaka la sita, siku na mahali hapo mshtakiwa Veronika akiwa na nia ovu alijipatia mkopo wa Sh25milioni kupitia akaunti yake  iliyopo katika benki hiyo kwa njia ya udanganyifu baada ya kuwaonyesha leseni ya biashara na leseni ya gari kama dhamana ya mkopo huo huku akijua kuwa siyo kweli.

Katika shtaka la saba mshtakiwa Veronika anadaiwa kutakatisha fedha kiasi cha Sh25milioni huku akijua kuwa pesa hizo ni zao la makosa ya kughushi.

Hata hivyo, washtakiwa wamekana makosa hayo na mshtakiwa Lilian ameachiwa kwa dhamana huku Veronika akirudishwa rumande kwa kuwa shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana

Hakimu Rwizile aliahirisha kesi hiyo hadi, Julai 2, mwaka huu itakapotajwa.