Waziri Kigwangalla: Tumuache Konki Liquid apate riziki yake

Muktasari:

  • Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema kila mtu anayo fursa ya kufanya kile anachokipenda na katika maisha kila mtu ana aina yake ya kufikia ndoto zake

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema wanaombeza Peter Molel maarufu Konki Liquid 'Pierre', wanakosea kwani kila mtu ana kusudi la kuwepo duniani na anachokifanya Mtanzania huyo ni kuwapa faraja wengine.

Dk Kigwangalla ametoa kauli hiyo  kupitia ukurasa wake wa Instagram ikiwa ni siku mbili tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuzungumza katika halfa ya Tokomeza Zero Kisarawe, kauli iliyozua utata mitandaoni kuhusu Konki Liquid huku akimuita mtu wa hovyo.

"Ningewasihi sana waandishi wa habari akina mama kama hawa ndiyo wapewe kipaumbele siyo hao walevi walevi hao akina Pierre sijui akina nani, yaani unakuwa na taifa ambalo watu wa hovyo ndiyo wanakuwa maarufu halafu watu wa maana hawajulikani walipo…" alisema Makonda.

“Kwa Pierre Liquid kufanya anachofanya na kufurahisha wanaoona ‘anachekesha’. Nchi haiwezi kujengwa na watu wanaofanya mambo magumu magumu pekee. Kila mmoja wetu anafanya sehemu yake. Pierre anatuchekesha na kutukumbusha kufurahia maisha tunapopata nafasi, haswa tunapotoka kufanya hayo mambo yetu magumu magumu!” Aliandika.

Waziri Kigwangalla amesema maisha ni magumu, yana mitihani mingi na ni mafupi, katika kuleta furaha na shangwe kwenye maisha ndiyo maana ‘wachekeshaji’ wakapata ajira! Wengine wasome udaktari, uhandisi na wafanye uvumbuzi na utatuzi wa changamoto na wengine watetemeshe, wavuruge akili, watoe raha na furaha, wachekeshe, siku zisogee.

“Maisha ndiyo haya haya! Zaidi ya yote, Pierre ni mtu huru kwenye nchi yake. Tunapaswa kuulinda uhuru wa Pierre kama ambavyo Katiba ya nchi yetu inavyoelekeza. Let him be. Tumuache apate riziki yake. Mungu anajua zaidi kwa nini hatukumjua miaka mitano iliyopita na kwa nini sasa anazua mjadala,” ameandika Kigwangalla na kuongeza;

“Hata kwa mimi binafsi, Mungu anajua zaidi kwa nini sikuwa Waziri miaka mitano iliyopita na leo ni Waziri. Mungu anatupangia maisha yetu. Anatugawia mafungu yetu. Pengine hii inaweza kuwa sababu ya Pierre kuwa mtu bora zaidi leo kuliko ile siku aliyopiga ukelele wa raha na kubembea pale Liquid! Pengine hii ndiyo nyota yake ya jaha. Kwa hakika, Pierre atabaki kuwa juu! Pierre atabaki kuwa kileleni! #HK.”