Waziri Ndalichako awasimamisha watumishi sita chuo cha Patandi

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya watoto wenye mahitaji maalumu ya Patandi wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha leo,kulia ni Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha,Jerry Murro.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

 

  • Shule maalumu ya Sekondari Patandi itakapokamilika itakuwa ikipokea watoto wenye mahitaji maalumu ambayo wanafunzi wa chuo maalumu Patandi watakuwa wakiitumia kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.

Arusha. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewasimamisha kazi watumishi sita wa Chuo cha Elimu Maalumu Patandi Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kwa makosa mbalimbali yakiwamo uzembe, matumizi mabaya ya fedha za umma na upotevu wa vifaa vya ujenzi wa Sekondari Maalumu Patandi.

Akizungumza na uongozi wa chuo hicho leo Jumapili Februari 3, 2019, Profesa  Ndalichako amesema Serikali haiwezi kuwavumilia watumishi wazembe wanaokwamisha miradi ya maendeleo bila sababu za msingi.

Watumishi waliosimamishwa ni mhasibu mkuu, Rose Kijaka; makamu mkuu wa chuo, Isack Myovela; mwenyekiti wa kamati ya mapokezi, Peter Mosha; boharia wa chuo, Charles Njarabi; na Henry Matei aliyehamishiwa Chuo cha Ualimu Monduli ambaye ameagiza arudishwe kujibu tuhuma zinazowakabili.

Kuhusu mkuu wa chuo hicho, Janes Liana amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, kumuondolea madaraka na kuendelea na utumishi kutokana na maradhi yanayomsumbua kwa muda mrefu.

Pia, amemuagiza Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), kumchukulia hatua aliyekuwa msimamizi wa mradi huo, Israel Mayage kwa kushindwa kutimiza wajibu wake.

Profesa Ndalichako amechukua uamuzi huo baada ya kubaini ucheleweshaji wa ujenzi wa shule hiyo maalumu ambayo ilianza kujengwa Aprili  2017 hadi sasa haijakamilika, huku ikiwa imepangiwa kupokea wanafunzi 650 wenye ulemavu Februari 7, 2019.

"Haiwezekani shule moja ijengwe kwa karibu miaka miwili wakati fedha zipo na sioni thamani ya fedha kwa kazi iliyofanyika na watumishi wote waliosababisha tukafikia hapa tutawachukulia hatua za kisheria na ikibainika wamechukua fedha za umma mali zao zitataifishwa na mafao ya kustaafu," amesema Ndalichako.

Amesema kulingana na nyaraka zinaonyesha mifuko 8,500  ya Saruji imenunuliwa lakini kamati ya ujenzi inadai ni mifuko 6,500 tu ambayo nayo haiendani na kazi iliyofanyika.

Waziri huyo amesema makosa aliyoyabaini ni kuwapo ununuzi uliofanyika bila risiti hatua ambayo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) aligundua zaidi ya Sh237 milioni kutokuonyesha risiti zake.

Pia, katika ununuzi moja ya risiti inaonyesha Novemba 30, 2017 kiasi cha malori 170 ya mchanga yalinunuliwa wakati wajumbe wa kamati ya ujenzi wakiwa hawana taarifa.

"Sitakubali fedha za umma zipotee sioni thamani ya Sh990 milioni kwenye awamu ya kwanza na tayari tumeshatoa nyingine Sh1 bilioni, lazima tuwe wazalendo kwa ajili ya nchi yetu," amesema Profesa Ndalichako.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amesema kesho atakuwa na kikao  na kamati ya ujenzi kujiridhisha kama wana uwezo wa kusimamia kazi hiyo au awape kazi hiyo kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Oljoro.

Amesema atahakikisha kasi ya ukamilishaji wa madarasa, mabweni na bwalo vinakamilika kwa wakati ili kuruhusu wanafunzi kuanza masomo kwa wakati.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk AveMaria Semakafu amesema baada ya kubaini kasi ya ujenzi kutokuwa nzuri alimteua mkuu wa Wilaya ya Arumeru kuwa mwenyekiti wa ujenzi ili kufanikisha nia ya Serikali.