Waziri atoa siku 30, ataka kadi na vocha za TTCL kupatikana kwa wingi

Muktasari:

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Atashasta Nditiye amelipa siku 30 Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kuhakikisha maeneo ambayo hayana kadi na vocha za simu za mtandao huo, zinapatikana

 


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Atashasta Nditiye amelipa siku 30 Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kuhakikisha maeneo ambayo hayana kadi na vocha za simu za mtandao huo, zinapatikana.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 14, 2019 katika ziara ya kukagua utendaji kazi ya shirika hilo.

Amesema TTCL ni shirika la wananchi, hivyo wanapaswa kuona matunda yake moja kwa moja ikiwamo kupata huduma zake.

"Ninawapa mwezi mmoja kuitatua changamoto ya upatikanaji wa kadi na vocha kwenye maeneo ya vijijini na maeneo yote nchi mzima" amesema Nditiye.

Nditiye amefafanua kuwa shirika hilo limebuni  vitu vingi vinavyopaswa kusimamiwa kikamilifu ikiwamo mkutano kwa njia ya video.

"Mbinu hii imekuwa rahisi na imepunguza gharama, kuna wakati waziri mkuu amekuwa akiwasiliana na mawaziri kwa njia hii, kutoa maelekezo na yanafanyiwa kazi,” amesema Nditiye.

"Msirudi nyuma endeleeni kubuni vitu vingine ili mlikamate soko la mawasiliano hapa nchini.”

Mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo, Omary Nundu amesema wanataka kutumia miundombinu yao kufanya kazi.

“Changamoto zipo chache ambazo kimsingi zinafanyiwa kazi kuhakikisha zinamalizika, pia kuongeza matangazo ili wananchi watambue huduma zetu na kuzitumia, ”amesema Mhandisi Nundu.