Atuhumiwa kuua mtoto wa miaka mitatu kwa kumkata panga kichwani

Sunday February 17 2019

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Simon

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Simon Haule 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Shinyanga. Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Paskazia Andrew Sindano (17) kwa tuhuma za mauaji ya mtoto Kashindye Mgemagiko (03) kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.

Taarifa ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Simon Haule aliyoitoa leo Jumapili Februari 17, 2019 imeeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi Ijumaa saa 12 jioni katika kitongoji cha Emalaupena kijiji cha Misayu kata ya Ubagwe, halmashauri ya wilaya ya Ushetu.

“Chanzo cha tukio hili ni wivu wa kimapenzi kwa kuwa mama wa mtoto aliyeuawa inasemekana alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mume wa Paskazia na kupelekea kuzaliwa mtoto huyo,” amesema Haule na kuongeza kuwa mbinu iliyotumika ni kumkata panga kichwani nje ya nyumba yake.

Amesema kwa sasa mwili umehifadhiwa huku kamanda huyo akisema mtuhumiwa  atafikishwa mahakamani mara moja.

Kamanda Haule amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wapeleke malalamiko, kero na migogoro yao hususani ya kimapenzi katika ofisi za serikali ya kijiji na mabaraza ya wazee ili kuepuka vitendo vya kinyama.

MWISHO

Advertisement

Advertisement