Kubenea, Komu watinga makao makuu ya Chadema

Muktasari:

Wabunge wa Chadema, Antony Komu (Moshi VIjijini) na Saed Kubenea wa Ubungo ambao leo itatolewa hatima yao, wamewasili katika ofisi za makao makuu ya chama hicho kusubiri uamuzi wa kikao cha kamati kuu


Dar es Salaam. Wabunge wa Chadema, Antony Komu (Moshi VIjijini) na Saed Kubenea wa Ubungo wamewasili katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiwa ni muda mfupi kabla ya kutolewa taarifa rasmi kuhusu hatima yao.

Wabunge hao wamewasili kwa pamoja na kuingia moja kwa moja ndani  ya ofisi za chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Jana Jumatano, Oktoba 17, 2018 kikao cha kamati kuu cha dharura kilifanyika katika Hoteli ya Bahari Beach na kumalizika usiku wa kumkia leo Alhamisi kikiwa na ajenda moja ya kuwajadili wabunge hao.

Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja ya kuwahoji wabunge hao baada ya siku za hivi karibuni kuzua mjadala ndani na nje ya chama hicho kwa kile kinachodaiwa kuwa ni sauti yao iliyokuwa ikisikika wakipanga mpango hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John  Mrema amesema leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 kutakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia kile kilichojiri kwenye mkutano huo wa kamati kuu.

Tayari waandishi wamekwisha kuwasili makao makuu ya chama hicho huku Kubenea akitoka ndani  na kuanza kusalimiana na waandishi mbalimbali waliopo hapo.

Endelea kufuatilia Mwananchi