Lema ataka tume huru kuchunguza mauaji Kigoma
Muktasari:
- Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema leo Ijumaa Novemba 2,2018 amezungumza na waandishi wa habari na kushauri kuundwa tume huru kuchunguza mauaji baina ya raia na polisi katika wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma
Arusha. Mbunge wa Arusha mjini (chdadema), Godbless Lema ametaka tume huru kuchunguza mauaji yaliyotokea mkoani Kigoma ili kujulikana ukweli badala ya kuendelea kumshikiliwa kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe.
Zitto anashikiliwa na jeshi la polisi tangu juzi, kwa tuhuma za kutoa taarifa za mauaji ya raia katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma baina ya polisi na jamii ya wanyantunzu.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Ijumaa Novemba 2, 2018 ofisini kwake jijini Arusha, Lema amesema kuna utata juu ya idadi ya watu, waliouawa, wakati polisi ikisema raia ni wawili na polisi wawili, mbunge wa Kigoma Kusini (CCM) Hasna Mwilima anasema raia ni 17.
"Hapa kuna mgongano, hata kama ingekuwa amefariki mtu mmoja, thamani ya binadamu haipimwi kwa mtu mmoja, thamani ya binaadamu ni ubinaadamu wake hata kama ni kichaa," amesema
Lema ametaka taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari na wadau wengine, kutoa matako ya kulaani mauaji ya watu, kupotea watu kwani sasa hofu inalikumba taifa na wale wanaojitahidi kusema wanakamatwa.
"Hili la kukamatwa Zitto tunapaswa sote tukemee, Zitto siyo kibaka ni mbunge alikuwa anawasilisha maoni yake bila kuvunja sheria kwa nia njema ili serikali ifanye uchunguzi lakini amekamatwa," amesema.