VIDEO-Lipumba: Ukawa haiwezi kuitoa CCM

Muktasari:

  • Mazrui alisema kilio cha Watanzania walio wengi ni Ukawa na Profesa Lipumba anajua umoja huo ni sumu kwake na ndio utakaoiondoa CCM madarakani hivyo hashangai kuona akiupiga vita kwa kuwa anafanya hivyo kulinda masilahi yake na ya watu wachache.

Dar es Salaam. Profesa Ibrahimu Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF anayekubalika na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa amesema muungano wa baadhi ya vyama vya siasa kwa mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hauwezi kuiondoa Serikali ya CCM madarakani hivyo liundwe shirikisho jipya.

Alisema hayo jana alipokuwa akitoa mapendekezo ya kikao cha baraza la chama chake kilichofanyika Machi 17 na 18 ikiwa ni pamoja na kuitaka kamati ya utendaji kupitia na kuyafanyia kazi kwa kina maoni ya wananchi waliopoteza imani na ushirikiano uliopo ndani ya Ukawa ambao alisema, “Hauwezi kuiondoa Serikali ya CCM madarakani... Tunataka kutengeneza mpango wa mashirikiano mengine yatakayokuwa na tija na kuleta mabadiliko ya kweli kulingana na mahitaji ya kisiasa yalivyo sasa.”

Hata hivyo, kauli hiyo, imepondwa na Nassor Ahmed Mazrui ambaye ni naibu katibu mkuu wa CUF Zanzibar anayemuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad akisema Ukawa ndilo hitaji la wananchi.

“Yeye (Profesa Lipumba), alitoka ndani ya CUF sasa mambo ya Ukawa yanamhusu nini? Akae akijua Watanzania ndio wanaitaka Ukawa na huwezi kuwazuia, yeye yupo upande fulani kamwe hawezi kuunga mkono umoja huu,” alisema.

Mazrui alisema kilio cha Watanzania walio wengi ni Ukawa na Profesa Lipumba anajua umoja huo ni sumu kwake na ndio utakaoiondoa CCM madarakani hivyo hashangai kuona akiupiga vita kwa kuwa anafanya hivyo kulinda masilahi yake na ya watu wachache.

Akijibu hoja ya Maalim Seif kuwakumbatia viongozi wa Chadema, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema anachofanya Profesa Lipumba ni “kutafuta umaarufu ili kurudisha heshima yake kwenye ‘gemu’. Atambue kuwa kuitoa CCM ni suala la wananchi ila hayo ni maoni yake siwezi kulumbana wala kupingana naye.

“Naomba atambue hakuna mstaarabu na mwenye hekima duniani anayeshabikia mgawanyiko ila nashukuru kwa maoni yake,” alisema Dk Mashinji.

Akizungumzia madai ya Maalim Seif Sharif kuidhoofisha CUF, Profesa Lipumba alisema suala lake linashughulikiwa na Baraza la Uongozi ambalo alisema ndicho chombo cha mwisho cha uamuzi.

Alisema kama Maalim Seif angekuwa anahudhuria vikao vya baraza hilo lingekuwa limeshamchukulia hatua za kinidhamu, lakini kwa kuwa hafiki inakuwa vigumu ikizingatiwa kuwa kuna suala la kuhojiwa.

“Atashughulikiwa na kamati ya maadili na nidhamu, kwa kumpa nafasi ya kujieleza kabla ya kuchukua taratibu za kinidhamu, kisha wataleta kwenye Baraza Kuu la Uongozi kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema.

Kuhusu hilo, Mazrui alisema Profesa Lipumba hana ubavu wa kumshughulikia Maalim Seif kwa sababu siyo mwenyekiti halali wa CUF na kamati ya maadili anayoizungumzia haitambuliki.

“Hana uwezo kwa sababu Baraza Kuu lake ni ‘feki’ ndio maana hana ajenda kila kukicha anamtajamtaja Maalim Seif tu,” alisema Mazrui.

Pia, Profesa Lipumba aliendelea na madai yake ya mara kwa mara kwamba Maalim Seif ameidhoofisha CUF kwa kuwakumbatia viongozi wa Chadema na kutotekeleza azimio la Baraza Kuu la kufungua kesi Mahakama Kuu ya Zanzibar kupinga kufutwa matokeo ya uchaguzi wa wawakilishi na madiwani ambao alisema walikabidhiwa hati za ushindi wa majimbo na Shehia zao baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Kesi hizo zingefunguliwa CUF ingekuwa na wawakilishi 27 wa majimbo na nusu ya wawakilishi wote wa viti maalumu, “Idadi ya hiyo ingekuwa sawa na idadi ya wawakilishi wa CCM, hivyo Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar ingekuwa na mawaziri wa CUF, hivi sasa wamebaki peke yao ndani ya Baraza la Wawakilishi na wanatunga sheria watakavyo.”

Alisema madhara ya hatua hiyo ni kubadilisha sheria ya uchaguzi, ambayo imeweka utaratibu wa wasimamizi wa uchaguzi na askari wanaolinda usalama kupiga kura siku moja kabla ya uchaguzi, “Kama wawakilishi wetu wangekuwa ndani ya Baraza hilo sheria hiyo isingepita.”