Maisha yanaendelea nje ya CCM, Lowassa awaambia wanaotimuliwa

Muktasari:

  • Lowassa ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa CCM katika baadhi ya wilaya umefutwa, huku wagombea walioonekana kumuunga mkono, wakiondolewa majina yao.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa amewataka wanachama wanaokatwa majina yao katika uchaguzi unaoendelea ndani ya CCM kujiunga na upinzani akisema kuna maisha nje ya chama hicho.

Lowassa ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa CCM katika baadhi ya wilaya umefutwa, huku wagombea walioonekana kumuunga mkono, wakiondolewa majina yao.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari jana, Lowassa anasema: “Nimesoma na kusikia baadhi ya waliokuwa viongozi katika Chama cha Mapinduzi wamekatwa ama kutetea nafasi zao au kugombea, kwa sababu mbalimbali. Na jina langu limekuwa likiendelea kutajwa tajwa humo.

“Mimi nawaambia hawa Watanzania wenzetu waliokatwa huko CCM, nawakaribisha huku Ukawa wafurahie demokrasia. Huku niliko kuna maisha mazuri ya kisiasa, uhuru wa fikra na demokrasia halisi.”

Lowassa alisema Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere alisema ni wakati muafaka kwa Tanzania kuwa na mfumo wa vyama vingi, pamoja na kwamba maoni ya Watanzania wengi wakati ule yalitaka mfumo wa chama kimoja, “Nataka kuwakumbusha Watanzania wenzangu hawa, uamuzi ule wa Baba wa Taifa ulilenga kuwapa Watanzania demokrasia ya kuwa na uwanja mpana wa kufanya siasa.

“Mimi nimetumia fikra hizo za mwalimu na hakika hivi sasa ninafurahia demokrasia halisi huku niliko. Kwa wote waliokatwa na wanahisi wameonewa waondokane na unyonge wa fikra kudhani kuwa bila CCM hakuna maisha... waje huku tufanye siasa kwa manufaa ya wananchi wetu.”

Lowassa amewaomba wana-Chadema wenzake kuwapokea kwa mikono miwili huku akiwaambia wanaoendelea kubaki CCM kuwa wataona makucha ya upinzani mwaka 2020.

“Vitisho na nguvu ya dola inayotumika kujaribu kutunyamazisha sisi wa upinzani, visiwakatishe tamaa wala kuwaogofya hata mara moja,” amesema Lowassa.