Majibu ya Lugola kuhusu mahabusu yawaibua wadau wa haki za binadamu

Muktasari:

  • Sakata hilo lilianzia bungeni jana baada ya Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji kuihoji Serikali kuhusu mkakati wake wa kukomesha matukio ya mahabusu wanaodaiwa kufariki dunia wakiwa mikononi mwa polisi.

Dar es Salaam. Majibu ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuhusu mahabusu wanaofariki dunia wakiwa mikononi mwa polisi, imezua mjadala ikipingwa vikali na wanasheria na watetezi wa haki za binadamu.

Sakata hilo lilianzia bungeni jana baada ya Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji kuihoji Serikali kuhusu mkakati wake wa kukomesha matukio ya mahabusu wanaodaiwa kufariki dunia wakiwa mikononi mwa polisi.

Akijibu swali hilo, Lugola alisema suala la mtu kufa halichagui mahali anapotakiwa kufia kwani kifo ni mtego.

Waziri Lugola ametumia kitabu cha Biblia katika Mhubiri 9 akinukuu kuwa kifo ni mtego na kila mtu amewekewa.

Alisema kifo ni ahadi ya Mungu na mtu anaweza kufariki mahali popote. “Wengine wanaweza kufia kwenye magari, hospitali, bungeni na hata wengine wanakufa kwenye nyumba wakijamiiana, je huko nako kuna nini,” alisema Lugola.

Lugola alikwenda mbali na kuwataka wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi kwa kuchoma vituo vya polisi inapotokea mtuhumiwa kafia kituoni kwani kama watafanya hivyo mbona hawachomi vitanda na nyumba wanazofia watu wakijamiiana?

Baada ya kusema hayo, Spika wa Bunge, Job Ndugai akasema: “Mheshimiwa Khatib, umeyataka mwenyewe.”

Wakipinga kauli ya Lugola Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Onesmo Olengurumwa walisema Waziri asitafute visingizio badala yake afanyie kazi hoja ya msingi. “Maneno yake hayana mantiki kwa sababu kulinganisha matukio mawili tofauti. Polisi wanatakiwa kuhakikisha usalama wa watu waliowashikilia kwa mahojiano na kulinda usalama ndilo jukumu lao,” alisema. “Ukizungumzia nyumba ya wageni ni tofauti kabisa kwa sababu hakuna mtu mwenye jukumu la kulinda usalama wa wateja wala kuangalia iwapo atashambuliwa au kuuawa, Polisi ni jukumu lao la msingi,”alisema.

Henga alifafanua kuwa shida kubwa kwenye uchunguzi wa matukio hayo ni kuwatumia Polisi kufanya hivyo badala ya timu huru kama ambavyo sheria inaelekeza.

Kwa upande wake Olengurumwa alisema waziri hakuwa na haja ya kuhamasisha wananchi kuchukua sheria mikononi.

Alisema kauli hiyo inahamasisha wananchi kuchukua sheria mkononi iwapo itatolewa taarifa ya mtu kufia kwenye nyumba za wageni au kwingineko tofauti na Polisi. “Alipaswa kukemea, badala ya kuhoji kwa nini wananchi hawachukui hatua kwa vifo vinavyotokea mahali pengine ikiwamo kwenye nyumba za wageni, ”alisema Ngurumwa.

Alisema wananchi wanahoji na wanakuwa na chuki na Polisi kutokana na vifo vya ndugu zao vinavyosababishwa na matumizi ya nguvu yanayofanywa na watunza usalama.

Alifafanua kuwa wanahisi nguvu hizo zinatumika kuwalazimisha kukubali mashtaka waliyotuhumiwa kuhusika.

Hivi karibuni kumekuwa na matukio kadhaa ya wananchi kususa maiti za ndugu zao au kuvamia vituo vya polisi baada ya ndugu zao kufariki mikononi mwa polisi. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na lile la Mbeya ambapo ndugu wa marehemu, Frank Kapange wamesusa kuchukua mwili wake tangu alipofariki kati ya Juni 4 na 5 mwaka huu akiwa mikononi mwa polisi. Mpaka sasa ndugu hao hawajazika.

Tukio jingine ni la Agosti mwaka huu, ambapo familia ya Kandamba iligoma kuchukua mwili wa ndugu yao, Salum Kandamba anayedaiwa kupigwa risasi na polisi tangu Agosti 11 jijini Dar es Salaam. Hata hivyo ndugu hao walikubali kuzika Agosti 29 baada ya kuzungumza na Waziri Lugola. Machi mwaka huu, wakazi wa Kata ya Iyela walizusha tafrani kubwa kutokana na kifo cha kijana Allen Mapunda, 22, anayedaiwa kufariki saa chache baada ya kuachiwa kutoka kituo kikuu cha polisi Mbeya alipokuwa akishikiliwa.