Lulu, bilionea Msuya na Bongo movie

Muktasari:

Ndipo katika maongezi Chusa akamdokeza Shariff kuwa kuna jambo anaomba afanye. Na kwamba, hata kuwepo kwake ndani ni njama za Msuya. Baada ya makubaliano hayo mchongo mzima ukaanza kusukwa. Na katika kusuka Chusa alimwambia Shariff (mshtakiwa wa 1), kwamba ukifika Arusha mjini mtafute Swahibu (mshtakiwa wa 2), ambaye leo kachomoka atakupa ramani yote na kinachotakiwa kufanyika. Ila wewe utafadhili zoezi zima.

Sinema ilianzia Gereza la Babati. Shariff Mohamed alienda kumtembelea Chusa, ambaye kwa wakati huo alikuwa mtuhumiwa katika kesi ya mauaji yaliyotokea katika mgodi wake.

Ndipo katika maongezi Chusa akamdokeza Shariff kuwa kuna jambo anaomba afanye. Na kwamba, hata kuwepo kwake ndani ni njama za Msuya. Baada ya makubaliano hayo mchongo mzima ukaanza kusukwa. Na katika kusuka Chusa alimwambia Shariff (mshtakiwa wa 1), kwamba ukifika Arusha mjini mtafute Swahibu (mshtakiwa wa 2), ambaye leo kachomoka atakupa ramani yote na kinachotakiwa kufanyika. Ila wewe utafadhili zoezi zima. Swahibu Jumanne maarufu kama Mredii, kwa uzoefu wake akamtafuta Kuhundwa na Ally Majeshi. Ally Majeshi akatoa wazo kuwa Shariff atoe jiwe kisha akamuoneshe Msuya kuwa analiuza. Shariff akakubali.

Na mchongo ukawa ndio huo. Shariff akatoa jiwe lenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni na kumpa Majeshi. Majeshi alimpigia Msuya akamwambia anaitwa Ally anatokea Mirerani kuna jiwe kapata. Anaomba waonane ili amwonyeshe. Msuya akakubali na kumwambia wakutane mjini Arusha. Ilikuwa mida ya jioni saa 11, walikutana na Majeshi alimwonyesha jiwe Msuya, akalipenda, akasema atatoa Sh140 milioni.

Majeshi akakubali ila akamwambia hiyo biashara yuko na mdogo wake, hivyo ni vyema mauziano yafanyike wakiwa wote wawili na mdogo wake. Msuya akakubali.

Kwa hiyo wanafanyaje? Majeshi akasema kesho kama anaweza wakutane njiapanda ya Kia ili na mdogo wake pia awepo asione amemdhulumu. Msuya akakubali.

Huku maandalizi mengine yalikuwa yanaendelea. Line za simu zilisajiliwa Moshi mjini, line tatu kwa kutumia jina la Kimasai. Na aliyefanya kazi hiyo ni mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu na aliyekuwa mshtakiwa wa saba alichomoka na Ally.

Siku ya tukio asubuhi walikutana Shamo Hotel. Kisha wakakubaliana kuwa Kuhundwa atatumia bodaboda kutokea njiapanda. Shariff alibaki njia panda na wengine. Ally Majeshi alipakiwa na Msuya kutoka Arusha.

Kumbuka hapa anafuatwa mdogo wake Majeshi ili mauziano yaweze kufanyika.

Walipofika njiapanda wakakunja kuelekea alipo mdogo wake Ally Majeshi. Walipofika tayari Kuhundwa alikuwa keshafika eneo la tukio.

Ally akashuka kwenye gari kama anaongea na Kuhundwa (mdogo wake kwa wakati huo). Msuya kabla hajashuka kwenye gari, Kuhundwa alifika na kufungua mlango kisha kuanza kumimina risasi.

Kisha wakakamata bodaboda na kuanza kuondoka eneo hilo. Shuhuda pekee alikuwa kijana mmoja wa Kimasai wa miaka 18 aliyekuwa anachunga mifugo yake eneo hilo.

Mussa Mangu ambaye ni dereva wa Shariff Mohamed, Kuhundwa, na Ally Majeshi siku moja kabla walienda Namanga kununua bunduki, ambapo ilinunuliwa kwa Sh4 milioni. Na gari lililotumika kwenda ni la Shariff Mohamed aina ya VX. Katika malipo ilikuwa imebaki kama Sh10 milioni. Ally na Kuhundwa walipofika njiapanda, wakaiweka pikipiki kwenye gari na kuelekea Arusha. Walipofika Arusha, Shariff aliwamalizia hela yote Sh10 milioni iliyobaki.

Hapo sasa maisha ya kawaida yaliendelea kwa mwezi mmoja mpaka miwili, kabla ya zoezi la kuwakamata mmoja baada ya mwingine kuanza rasmi.

Kuhundwa alikamatwa Kaliua akiwa kwa mganga wa kienyeji. Polisi walioenda kumkamata walikaa kama siku tatu wakiwa wanatibiwa wote, kumbe walikuwa kazini.

Ally alikamatwa Kigoma. Alipofika Mwanza mnara ulisoma yuko mjini Mwanza, kisha akazima simu akaja kuiwasha akiwa anavuka Busisi. Mnara ukasoma tena.

Wakasema huku anaelekea Geita au mikoa ya huko. Baada ya hapo mnara ukaja kusoma Kigoma, ndipo polisi waliokuwa katika ‘task force’ walifika Kigoma. Kwa siku mbili zote hawakufanikiwa kumkamata. Baada ya kukata tamaa wakiwa kwenye gari wanarudi, wakasema tupite stendi kupata kifungua kinywa.

Walipokuwa stendi, mmoja wa askari akamuona mtu kama Ally. Alipojaribu kupiga ile namba Ally akapokea ndipo akamakamatwa. Shariff Mohamed alikamatwa Arusha baada ya kurudi kutoka safari. Saa 11 alfajiri alisikia watu wakigonga kengere ya getini. Alipochungulia katika kamera ya CCTV akaona kuna polisi, kisha akafungua geti na kukamatwa.

Chusa alikamatwa na kukaa ndani zaidi ya miezi sita katika kesi hii ya Msuya, kisha DPP akaonyesha nia ya kumuondoa Chusa katika hili shauri na kwamba hata kesi ya mauaji inayomkabili kwa sasa ni Msuya ndiye alitengeneza. Shariff anazidi kusema kwamba, kwa kuwa Chusa ni rafiki yake, na wanafanya naye biashara na ni rafiki mkubwa hakuweza kukataa ombi hilo.

Ingawa alimuomba muda afikirie, Shariff anasema alipofikiria aliona kwamba Chusa akitoka anaweza kumuua yeye. Hivyo alikuwa hana jinsi zaidi ya kukubali hilo ombi la Chusa.

Ndipo idadi ya washtakiwa ikabaki saba. Mmoja akachomoka awali alipoonekana hana kesi ya kujibu. Wengine sita ndio wamehukumiwa. Watano wamehukumiwa kunyongwa na mmoja kachomoka ambaye ni Swahibu Jumanne maarufu kama Mredii.

Hizi nd’o stori za kufanyia kazi wasanii wa filamu. Badala ya mvulana wa kimaskini kapendwa na msichana wa kitajiri. Au mwenye nyumba kulazimisha penzi la mpangaji.

Kuna matukio ambayo wasanii wameshindwa kugeuza pesa, yanakuja na kutoweka kama upepo halafu basi stori inaisha juu kwa juu huku filamu zikitengenezewa kwa stori za vituko.

Hivi sasa utawaona pamoja misibani. Huko ndiyo utasikia habari za wasanii na vitimbi vyao. Zaidi ya hapo huwasikii. Bila misiba wengine tusingewaona tena runingani.

Leaders Club yao ya sasa, ndiyo ‘location’ yao. Ndiyo kwenye mauzo yao rasmi. Itafika wakati mashabiki wataomba misiba iwe mingi wapate nafasi ya kuwaona wasanii wanaowapenda.

Wapo wasanii wanaotumia misiba kutengeneza ‘kiki’ ya kazi zao mpya. Kutumia misiba kama sehemu ya kutangazia ujio wa kazi yako mpya ni hatua mbaya sana. Biashara kubwa ya wasanii wa filamu ilikuwa ni mauzo kwa Mdosi, lakini sasa hivi hilo halipo tena limekufa kabisa. Sanaa inayumba kwa kuwa wasanii hawakujipanga jinsi ya kuishi nje ya biashara na Mdosi.

Huyo ndiye aliyekuwa mwokozi mkubwa aliyebaki. Leo kila msanii anasifia tamthiliya na kukimbilia huko. Sasa sijui itakuwaje kama na huko nako kutaharibika.

Wasiwasi wangu unakuja kwa sababu wasanii wanaoshindwa kuvumilia ‘location’ kwa filamu za dakika chache, watawezaje kazi ya miezi mingi? Matatizo ya wasanii kutotulia wawapo ‘location’ ni makubwa sana.

Kuna wakati wasanii wa Kibongo walijifananisha na wa Kinaijeria mpaka jina la Bongo movie wakataka lifanane na Nollywood, ikashindikana kwani kujiita Bollywood ni kichekesho kwa sababu India kuna Bollywood.

Nollywood ilianza kupata umaarufu mwanzoni mwa miaka ya 1990 mpaka mwaka 2000 ikawa ya pili kuzalisha filamu nyingi kwa mwaka baada ya Bollywood.

Walikuwa wakizalisha filamu 200 kwa mwezi, sawa na filamu 2,400 kwa mwaka. Nigeria na Tanzania wana historia sawa katika filamu. Wote walianza kutengeneza filamu mwanzoni mwa miaka ya 1960.

Kwa Tanzania filamu ilianza kabla ya uhuru yaani mwaka 1961, lakini mwaka 1968 ilianzishwa taasisi ya Tanzania Film Festival. Walifanikiwa kutengeneza filamu za Fimbo ya Mnyonge, Harusi ya Mariamu na Yombayomba.

Miongoni mwa filamu zilizopata umaarufu ni ‘Muhogo Mchungu’ iliyomshirikisha Rashid Mfaume Kawawa ambaye alikuwa Waziri Mkuu wakati Tanganyika ikipata uhuru.

Hizo filamu zilitumika kwa propaganda na sera ya ujamaa na kujitegemea. Ilipofika mwishoni mwa miaka ya 1990 ndipo utamaduni wa kutengeneza filamu kwa minajili ya kibiashara ukaanza rasmi.

Ili kurudisha ubora ule wa soko la Bongo movie kuna kazi kubwa inatakiwa ifanyike. Wala siyo suala la kuwekeza mtaji mkubwa wa mamilioni. Ni kurudisha imani ya mashabiki kwenu.

Anaweza kutumika msanii mmoja au wawili kurudisha imani ya mashabiki kama mwanzo. Biashara nyingi zimekufa au kuyumba kwa sasa lakini pia kuna biashara nyingi zimezaliwa au kusimama vizuri kwa sasa.

Watanzania wanapenda sana faraja. Filamu ni faraja kubwa sana lakini kwa sasa kiwanda cha sanaa hii kinahitaji kupata akili mpya siyo hizo za zamadamu. Watu wanaishi kwa mazoea na kukariri mno.

Wasanii ondokeni kwenye akili za kutengeneza stori za filamu kwenye mawazo ya baa. Kuna matukio mengi sana yanayojiri kwa uwazi na kwa kificho yanayohitajika kuwekwa kwenye filamu zenu.

Maisha ya Elizabeth Michael ‘Lulu’ ni filamu tosha. Lakini hilo haliwezi kuonekana kwenye akili za watu wanaofikiria zaidi kuuza sura kwenye misiba na kubishana na mashabiki wao mitandaoni.