‘Muswada umempa msajili mamlaka yaliyopitiliza’

Wakati Muswada wa Sheria ya vyama vya Siasa ukitarajiwa kusomwa mara ya pili katika bunge lijalo, umeelezwa kuwa ni mwendelezo wa kusinyaa kwa demokrasia na ukandamizwaji wa haki za binadamu.

Muswada huo uliopo katika hatua ya mjadala wa umma ukipita na kuwa sheria, itakuwa ni miongoni mwa sheria kadhaa zilizopitishwa miaka ya karibuni zinazobana demokrasia na uhuru wa kujieleza.

Wadau wanaiona sheria hiyo kama inakwenda kufuta mfumo wa vyama vingi uliorejeshwa mwaka 1992.

Hata hivyo, mara kadhaa Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa imekuwa ikitoa ufafanuzi wa utata wa muswada huo ikisema ilishirikisha vyama vya siasa wakati wa kuuandaa.

Katika kujadili muswada huo, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kimefanya kongamano hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambapo, mwasilishaji wa mada, Wakili Harold Sungusia aliweka bayana kuwa sheria hiyo inajichanganya ikimpa madaraka makubwa mno Msajili wa vyama vya siasa.

“Msajili anaweza kuamua usajiliwe au usisajiliwe, ufutwe au usifutwe, uwe mwanachama au usiwe, unafaa kuwa mgombea au hufai, aina gani ya elimu ya uraia inayotakiwa na nani aitoe, upewe ruzuku au usipewe,” alisema Sungusia.

Alihoji: “Je, akimfuta uanachama Rais? Yaani msajili ana mamlaka kuliko Rais. Ni jambo kubwa la kikatiba.”

Anaendelea kutaja kifungu kinachompa kinga msajili, kwamba tofauti na sheria ya sasa ambayo angeweza kushtakiwa kwa makosa ya uzembe, kwa muswada mpya msajili hashtakiwi kabisa.

Sungusia alihoji pia uhalali wa waziri kuachiwa mambo mengine ya kimaamuzi katika kutunga kanuni, akisema naye hatatenda haki kwa kuwa naye anatoka chama kimojawapo cha siasa.

Kuhusu vyama vya siasa kuzuiwa na muswada huo kufanya harakati, Sungusia anasema hata chama cha Tanu kilifanya harakati hadi uhuru ukapatikana.

“Sasa vyama vitakuwa kwaya za siasa. Kazi ya chama cha siasa ni kuchukua madaraka, huchukui madaraka kwa kuimba pambio. Hata Tanu waliwashinikiza wazungu wakatoa madaraka,” alisema.

Suala la kinga kwa Msajili limemgusa Rais wa TLS, Fatma Karume akisema muswada huo unakwenda kinyume na Katiba.

“Watu wanaopewa kinga wanavunja Katiba ya Tanzania. Kwa sababu kwenye ibara ya 13(1) inasema, ‘Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki kulindwa na kupata haki mbele ya sheria.”

Anasema kinga imetolewa kwa watu wachache kwa mipango fulani, kama majaji wakiwa wanatoa uamuzi mahakamani na Rais naye amepewa kinga hiyo.

“Hatuwezi kuwa na Katiba inayosema kila mtu yuko sawa mbele ya sheria, halafu anatoka mtu huko anatunga sheria inayomweka mtu juu ya sheria,” anasema Karume.

Mwenyekiti wa chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa anazungumzia suala hilo alisema, “Hali itakuwaje, siku msajili amekwenda kwao Muleba huko, ameandika tangazo huko, kuanzia leo Rais si mwanachama, akatuma katika mtandao? Nchi itakuwaje?” alihoji Dovutwa.

Baadhi ya wanajopo waliojadili sheria hiyo akiwasmo askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) anasema muswada huo hauakisi matakwa ya vyama vya siasa bali matakwa ya ya msajili.

Naye msomi maarufu, Dk Azaveli Lwaitama amegusia mamlaka ya Msajili akisema ni mwendelezo wa utamaduni wa watu kupenda madaraka.

“Mamlaka ya msajili, nyuma ya pazia wameongeza vyeo kama wakurugenzi. Nyuma ni dola. Unajua madaraka ni matamu,” anasema Dk Lwaitama.

Kuhusu haki za wanawake, mhadhiri wa sanaa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Vicencia Shule amesisitiza umuhimu wa muswada huo kuwashirikisha wanawake kushiriki siasa kama wanaume.

Nini kifanyike?

Wakili maarufu wa Zanzibar, Awadhi Said anasema yanapokuwapo madai fulani kuhusu demokrasia, dawa yake siyo kuidhibiti bali ni kuiongeza.

“Unapotaka kujenga demokrasia ongeza tu, wakitaka kufanya mikutano mara ya mbili waambie waongeze mara nne au mara sita, watachoka tu.”

Akitoa maoni yake, Sheikh Issa Ponda anawataka wabunge kutofanya makosa kupitishwa muswada huo.

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika anaishauri TLS kuhakikisha muswada huo hauingii bungeni.

“Ni vema wadau wengine mlioshiriki mkutano huu mkashirikisha taasisi nyingine za dini na kiraia, ziende kwa wingi mbele ya kamati ya Bunge zihakikishe kwamba huu muswada hauendi mbele ya Bunge, uondolewe,” alishauri Mnyika.

Mbunge wa Kigoma Mjini alisema muswada huo usichukuliwe kama wa vyama tu bali unagusa maslahi ya watu wote.

“Mimi nawaomba na ninashukuru TLS kwa kuona huu muswada si wa vyama tu. Vyama vya siasa ndiyo wasemaji wa wananchi kikatiba maana mgombea binafsi haruhusiwi. Ukishapitishwa muswada huu unaodhibiti vyama na wabunge, mtasemea wapi? Nani atawatetea?” alihoji Zitto.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole anautetea mchakato wa muswada huo akiwataka wapinzani kutowatisha wananchi.

“Tusianze kutishwa katikati ya mchakato, tusianze kujenga taswira ya kukataza kuvuka mto kabla hatujafika darajani. Sasa hivi tunazungumza ndiyo maana tumepewa nyaraka, tuachwe tuzungumze tusitishwe kwa kuweka kauli timilifu.