Tuzo ya Nobel ya uchumi ina maana kubwa kwa Tanzania

74019UchumiWashindi wa tuzo ya uchumi ya Nobel mwaka huu, William Nordhaus (Kushoto) na Paul Romer. Picha ya mtandao

Muktasari:

  • Tuzo ya Nobel hutolewa kila mwaka kuwatambua watu wenye mchango wa ziada kwenye jamii. Ingawa washindi wanaweza wasiwe wanatoka Tanzania, tuzo ya uchumi inawagusa Watanzania kwa namna moja au nyingine hasa kw akipindi hiki inapojipanga kujenga uchumi wa kati utalkaotegemea zaidi viwanda.

Kila mwaka hutolewa tuzo mbalimbai kitaifa na kimataifa kwa watu binafsi na taasisi. Kati ya tuzo maarufu kimataifa ni ya Nobel. Tuzo hii hutolewa kila mwaka kwa watu au taasisi zilizotoa mchango wa kipekee katika nyanja mbalimbali ukiwamo uchumi.

Kwa mwaka 2018 tuzo ya Nobel ya uchumi imeenda kwa wachumi; William Nordhaus na Paul Romer wa vyuo vikuu Marekani.

Tuzo ya Nobeli ni ya kimataifa inayotolewa na taasisi za nchini Sweden na Norway kwa kutambua mchango wa wapokeaji wa tuzo hii kwa uanazuoni, mila na maendeleo ya sayansi.

Msingi wake ni wosia wa mwanasayansi wa Sweden aitwaye Alfred Nobel. Wosia huu ulianzisha tuzo tano za Nobeli mwaka 1895. Hizi ni tuzo katika nyanja za fasihi, utabibu, fizikia, kemia, uchumi na amani. Tuzo hizi zilitolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1901. Hizi ni tuzo zenye heshima zaidi duniani.

Tuzo ya Nobel ya uchumi ni maalumu kwa kutambua mchango wa kipekee na wa hali ya juu wa mtu au taasisi katika tasnia ya uchumi.

Ilianzishwa mwaka 1968 kwa mchango wa Benki Kuu ya Sweden kwa taasisi ya Nobel wakati benki hiyo ikiadhimisha miaka 300 ya kuanzishwa kwake.

Tuzo hii haipo katika orodha za tuzo alizoanzisha Alfred Nobel mwaka 1895. Hata hivyo ipo chini ya tuzo nyingine zinazoandaliwa na kutolewa na taasisi ya Nobel.

Tuzo ya mwaka 2018

Tuzo ya Nobel ya uchumi kwa mwaka 2018 ilitangazwa Oktoba 8 ikiwa na thamani ya fedha za Sweden, Krona milioni tisa zilizogawanywa sawa kwa washindi hao wawili.

William Nordhaus wa Chuo Kikuu cha Yale Marekani aliipata tuzo hii kwa utafiti wake kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika uchumi wakati Paul Romer wa Chuo Kikuu cha Biashara NewYork, Marekani alipata tuzo hiyo kwa kuingiza masuala ya teknolojia na ubunifu katika uchambuzi data za muda mrefu za uchumi.

Wawili hawa wamebuni njia za kutatua changamoto za msingi za namna ya kuleta ukuaji uchumi wa muda mrefu ulioendelevu.

Wamepanua wigo wa uchambuzi wa uchumi kwa kutengeneza modeli inayoelezea namna uchumi wa soko unavyoingiliana na maumbile na ujuzi.

Mambo ya msingi katika tuzo hii ni muhimu katika hali ya Tanzania kama inavyoonyeshwa hapa.

Mabadiliko ya teknolojia

Teknolojia na mabadiliko yake ni muhimu katika ukuaji wa uchumi Tanzania na kwingineko. Katika utafiti uliompatia Romer tuzo ya Nobel, ameonyesha namna ambavyo ujuzi unaweza kutumika kusababisha na kuchochea ukuaaji wa uchumi kwa muda mrefu.

Romer ametoa mchango wake katika tasnia ya uchumi kwa kuonyesha namna nguvu za uchumi zinavyoweza kusababisha kampuni kuwa na utayari wa kuzalisha mawazo mapya na ubunifu.

Ameonyesha kuwa mawazo ni tofauti na bidhaaa na huduma nyingine za kiuchumi. Mawazo yanahitaji hali maalumu ili yaweze kuibuliwa, kuibuka na kukua hatimaye kuchangia katika ukuaji uchumi.

Ameleta msisimko mpya katika utafiti kuhusu udhibiti na sera zinazochochea mawazo mapya na ustawi wa uchumi wa muda mrefu.

Umuhimu wa teknolojia

Mabadiliko ya teknolojia kwa ujumla wake ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi Tanzania na duniani pia. Teknolojia ni muhimu katika kukuza uwezo wa wazalishaji bidhaa na huduma kuongeza wingi na ubora wa bidhaa na huduma wanazotoa.

Pamoja na teknolojia, washindi wa tuzo ya Nobel ya uchumi mwaka 2018 walifanya utafiti kuhusu mawazo na ubunifu. Pamoja na mambo mengine, walitafiti mazingira ya kisheria, kiudhibiti na kisera yanayotakiwa ili mawazo na ubunifu vizalishwe, vilelewe, vikue na kuchangia maendeleo kwa ujumla na ukuaji wa uchumi kimahususi.

Yote haya yanaihusu Tanzania kama yanavyozihusu nchi nyingine Afrika na kwingineko. Tanzania si kijiji, mabadiliko mazuri yanayotokea mahali fulani ianapaswa kujifunza.

Mabadiliko tabianchi

Nordhaus ameshinda tuzo ya Nobel kwa mchango wake kuhusu muingiliano wa jamii na mazingira. Amefanya utafiti huo tangu miaka ya 1970. Huu ni wakati ambao wanasayansi walikuwa na hofu kubwa kuhusu ongezeko la joto duniani na madhara yake.

Katika miaka ya katikati ya 1990 aligundua na kutengeneza modeli kuhusu uhusiano kati ya uchumi na tabianchi. Alitumia nadharia za fizikia, kemia na uchumi kugundua na kutengeneza modeli hii.

Pamoja na mambo mengine, modeli hii hutumika kupima matokeo ya hatua mbalimbali za kisera katika mabadiliko ya tabianchi.

Tabianchi na uchumi

Kuna uhusiano mkubwa na wa moja kwa moja kati ya mabadiliko ya tabianchi na uchumi. Shughuli za uchumi zinaathiri tabianchi kwa njia kadha wa kadha. Vilevile, mabadiliko ya tabianchi yanaathiri uchumi.

Kutokana na ukweli huu, mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kuzizingatia katika hatua mbalimbali za mwenendo wa uchumi. Hatua hizo ni pamoja na ubunifu, uchambuzi, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya shughuli mbalimbali.