Walimu 88,566 wanufaika na maktaba mtandao ya TET

Tuesday April 2 2019Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako

Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako amesema kuanzishwa kwa maktaba mtandao kutawalazimisha walimu waliokuwa hawatumii teknolojia ya habari na mawasiliano katika kufundishia, kuanza kutumia.

Alisema maktaba ni nyenzo muhimu itakayosaidia kumaliza tatizo la vitabu shuleni hasa vile vya maeneo ambayo vilikuwa vikichelewa kufika.

Akizindua maktaba mtandao inayofanya kazi chini ya Taasisi ya Elimu nchini (TET) wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Profesa Ndalichako alisema maendeleo ya sekta ya elimu yanaweza kwenda kwa kasi kama wadau wakiwamo walimu watafanya kazi kulingana na ukuaji wa sayansi na teknolojia.

Tayari maktaba hiyo imeshasajili walimu 88,566 kwa ajili ya kuitumia katika kujifunza na kufundishia.

“Sekta hii bila sayansi na teknolojia haiwezekani kwa hiyo walimu niwaombe tu mtumie maktaba hii kwa sababu ndiyo nyenzo muhimu kwenye kujifunza Tehama, nashukuru tunafungua maktaba hii wakati Serikali ikiwa imewekeza vifaa kama kompyuta kwa zaidi ya shule 500,” alisisitiza.

Aliitaka TET kusimamia vizuri na kuhakikisha vitabu vinavyoendelea kuchapishwa havina makosa yaliyowahi kujitokeza siku za nyuma.

Alisema wapo baadhi ya watu ambao wamekaa kutafuta makosa kwenye vitabu ili wakiyaona waichafue Serikali jambo ambalo bodi ya TET inapaswa kuwa nalo makini.

Awali Mkurugenzi wa TET, Aneth Komba alisema zipo faida nyingi za kuwapo maktaba mtandao kubwa ikiwa kurahisisha upatikanaji wa machapisho ya ziada, kiada, mihutasari, kiongozi cha mwalimu na moduli mbalimbali za kufundishia.

“Maktaba hii ni utunzaji wa kudumu wa vitabu na itapunguza gharama kubwa kwa shule katika kuendesha maktaba zao yaani badala ya kuwa na majengo makubwa, itahitaji vifaa vya Tehama tu,” alisema.

Dk Komba alisema kwa sasa wanawasiliana na kampuni za simu kuona namna wanavyoweza kuhakikisha kila eneo iliko shule kuna mtandao wa kutosha, ili kumaliza changamoto hasa vijijini.

Aidha, alisema wameingia mkataba na kampuni moja ya mfanyabiashara Reginald Mengi kwa ajili ya kusambaza vifaa vitakavyokuwa vinatumia nishati ya jua.

Alisema tayari walimu 88,566 wameshasajiliwa kupitia maktaba hiyo.

Tayari shule binafsi zitanunua vitabu katika maktaba mtandao kwa gharama isiyozidi 400,000 na kupewa kopi 48 za kiada na 2000 za ziada.

Advertisement